Joy FM
Joy FM
21 May 2026, 11:28

Matumizi sahihi ya mifumo ya serikali ni jambo muhimu katika kuhakikisha uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo na Serikali imekuwa ikiweka mifumo ya kisasa ya usimamizi wa fedha na manunuzi ili kurahisisha utendaji kazi, kudhibiti matumizi mabaya ya fedha za umma na kuongeza kasi ya utoaji wa huduma kwa wananchi
Na Mwandishi wetu
Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, CPSP Hassan Rugwa amewataka wataalamu wa hesabu na manunuzi kutumia mifumo ya serikali kwa usahihi ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao.
Akihitimisha kikao kazi cha siku tano kinachoendelea katika Ukumbi mpya wa Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko, Katibu Tawala Rugwa ameisema ni muhimu kwa wataalamu hao kuzingatia matumizi sahihi ya mifumo ya serikali pamoja na kujiandaa kisaikolojia ili kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na weledi.

Pia amewataka kuwajengea uwezo watendaji wa ngazi za kata na vijiji ili waweze kuelewa taratibu za manunuzi katika kamati mbalimbali zikiwemo za ujenzi, manunuzi na mapokezi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kakonko Kanali Evance Mallasa amesisitiza kuwa Halmashauri na miradi mbalimbali inawategemea wataalamu hao, hivyo wanapaswa kufuata kanuni na miongozo ili kuepuka kuchelewesha malipo au utekelezaji wa miradi bila sababu za msingi.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko, Ndaki Stephano Mhuli ameisema mafunzo hayo ni muhimu katika kuimarisha utendaji kazi wa halmashauri, hasa katika masuala ya manunuzi, hoja za ukaguzi na ufungaji wa hesabu kwa mwaka wa fedha 2025/2026.

Mafunzo hayo yanatarajiwa kuhitimishwa rasmi kesho Ijumaa tarehe 22 Mei, 2026.