Joy FM

Burundi, UNHCR kuwarejesha kwao wakimbizi wa Congo

21 April 2026, 08:43

Kambi ya wakimbizi ya Busuma iliyopo Burundi ambayo inahifadhi wakimbizi wa Congo, Picha na Bukuru Elias

Burundi inahifadhi makumi ya maelfu ya wakimbizi wa Kongo, wengi wao wakikimbia mapigano yaliyozuka mwishoni mwa mwaka uliopita kabla ya kutwaliwa kwa mji wa Uvira, wengi wao wakiwa wamehifadhiwa katika kambi za Cishemere na Busuma Ruyigi Mashariki mwa Burundi.

Na Bukuru Elias

Serikali ya Burundi kwa kushirikiana na UNHCR (Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia wakimbizi) imetangaza kuanza kwa mpango wa kuwarejesha kwa hiari wakimbizi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuanzia tarehe 23 mwezi huu wa Aprili.

Mpango huu unakuja wakati juhudi zinaendelea za kurejesha amani mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, licha ya kwamba hali ya usalama bado ni tete katika baadhi ya maeneo.

Wakimbizi kutoka Congo waliopo katika kambi huko Burundi wakiwa wanachukuliwa taarifa kwa ajili ya kurejeshwa kwao, Picha na Bukuru Elias

Maafisa wamesisitiza kuwa kurejea huko kutakuwa kwa hiari kabisa, bila shinikizo lolote kwa wakimbizi.

Katika hatua ya kwanza, kipaumbele kitapewa makundi yaliyo hatarini zaidi, yakiwemo familia zenye watoto wanaosoma, hasa wanaojiandaa na mitihani ya kitaifa, watu wenye ulemavu au mahitaji maalum, pamoja na baadhi ya watumishi wa umma.

Wakimbizi watakaorejea wataelekezwa hasa katika maeneo ya jimbo la Kivu Kusini, hususan Uvira na maeneo yanayolizunguka kama Fizi, Mboko pamoja na Bonde la Rusizi.

Maafisa wanasema uamuzi huu umechukuliwa kwa tahadhari kubwa kutokana na hali ya usalama ambayo bado si thabiti katika maeneo mengine.

Wakimbizi watakaokubali kurejea watapatiwa msaada wa fedha wa dola 30 kabla ya kuondoka, pamoja na msaada mwingine watakapofika, ukiwemo chakula, makazi ya muda na fedha za kujikimu.

Mpango huu utafanyika hatua kwa hatua, huku mamlaka zikiwataka wakimbizi kufuata tu taarifa rasmi ili kuepuka upotoshaji wa habari.