Joy FM
Joy FM
6 May 2026, 12:41

Kamati ya Uhakiki wa mikopo ya asilimia 10 katika Wilaya ya Kasulu imefanya zoezi la kuhakiki vikundi mbalimbali vilivyowasilisha maombi ya mikopo kupitia Halmashauri ya Wilaya hiyo, kwa ajili ya kutolewa katika kipindi cha robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2025/2026.
Na Emmanuel Kamangu
Wanufaika wa mikopo ya asilimia kumi katika Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu Mkoani Kigoma wametakiwa kurejesha mikopo hiyo kwa wakati ili kutoa fursa kwa vikundi vingine kuweza kukopeshwa mikopo hiyo inayotelewa kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya uhakiki wa mikopo ya 10% Wilaya ya Kasulu Bi. Theresia Mtewele, wakati kamati hiyo ilipofanya uhakiki wa maombi ya mikopo kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu kwa ajili ya robo ya tatu ya mwaka wa fedha ambapo amehimiza wanufaika kuwekeza na kukuza mitaji yao badala ya fedha watakazopewa kuzifanyia matumizi yasiyo akisi maendeleo.

Aidha Mwakilisha wa Kamanda wa Polisi Wilaya ya Kasulu, Mkaguzi Mdsaidizi wa Polisi, Willy Lupa amewataka waombaji wa mikopo hiyo kuitumia kwa malengo yaliyokusudiwa na kujiepusha na matumizi yasiyo na tija.

Kwa upande wake, Afisa Mwandamizi wa TAKUKURU Wilaya ya Kasulu Bw. Alpha Eliatosa, amewataka waombaji wa mikopo kuwa waaminifu katika kuhakikisha jamii nzima inaendelea kunufaika na fedha hizo.
Katika zoezi hilo kamati ya uhakiki wa mikopo imefanikiwa kutembelea vikundi vilivyopo katika kata za Kalela, Kigembe, Muzye, Nyakitonto, Nyatenda na Makere, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali kuhakikisha kuwa mikopo hiyo inaleta tija na kuwa chachu ya maendeleo kwa wananchi.