Joy FM
Joy FM
10 July 2026, 16:38

Huduma bora za afya ni msingi muhimu wa maendeleo ya jamii na kuanzishwa kwa huduma za upasuaji katika Hospitali ya Manispaa ya Kigoma Ujiji ni hatua kubwa inayoonyesha jitihada za Serikali katika kuboresha sekta ya afya na kusogeza huduma karibu na wananchi
Na Mwandishi wetu
Hospitali ya Manispaa ya Kigoma Ujiji iliyoko Wilaya ya Kigoma, imeandika historia kwa kufanya kwa mafanikio upasuaji wa kwanza wa dharura tangu kuzinduliwa kwa chumba cha upasuaji katika hospitali hiyo kwa kumzalisha mama mjamzito aliyepata uchungu pingamizi.
Upasuaji huo umefanyika Julai 09, 2026 ukiongozwa na Mganga Mkuu wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, Dkt. Hashim Mvogogo, akishirikiana na timu ya wataalamu wa afya wa hospitali hiyo, na kufanikiwa kumzalisha salama mama huyo watoto wawili mpacha wa kiume ambapo mama na watoto hali zao zinaendelea vizuri.

Akizungumza mara baada ya kufanya upasuaji huo,Dkt. Mvogogo ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutoa fedha Shilingi Milioni 503 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la upasuaji na na vifaa tiba vyenye thamani ya Shilingi Milioni 400 ambavyo vimewezesha hospitali hiyo kuanza kutoa huduma za upasuaji.
Amemshukuru pia Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Dkt. Rashid Chuachua na Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma/Ujiji Kisena Mabuba, kwa usimamizi mzuri tangu kuanza kwa ujenzi wa jengo la upasuaji hadi kufikia hatua ya kuanza kutoa huduma.
Aidha ametoa wito kwa Wananchi kuitumia Hospitali ya Manispaa ya Kigoma/Ujiji, kwa huduma za matibabu akieleza kuwa hospitali hiyo ina wataalam pamoja na vifaa vya kisasa vinavyowezesha utoaji wa huduma bora za matibabu.

Kuanza kutolewa kwa huduma za upasuaji kwa wajawazito katika Hospitali ya Manispaa ya Kigoma Ujiji, ni hatua muhimu katika kuboresha upatikanaji wa huduma za afya kwa Wananchi.