Joy FM

RC Kigoma ataka wananchi kutoa ushahidi vitendo vya ukatili Kasulu

10 October 2025, 12:32

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Balozi Simon Sirro akisalimiana na wananchi Wilaya ya Kasulu, Picha na tovuti ya Mkoa wa Kigoma

Serikali imesema kuwa itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo katika kutoa elimu na hamasa kwa wananchi ili waweze kushiriki katika mikakati ya kutokomeza vitendo vya ukatili kwenye jamii.

Na Mwandishi wetu

Wananchi Wilayani Kasulu Mkoani Kigoma wametakiwa kuwa tayari kutoa ushahidi pindi matukio ya vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto vinapotea ili hatua ziweze kuchukuliwa kwa wahusika wa vitendo hivyo.

Kauli hiyo imetolewa na MKuu wa Mkoa wa Kigoma Balozi Simon Sirro wakati akizungumza mara baada ya kukagua hali ya utendaji kazi wa dawati  la Jinsia na watoto katika Kituo cha Polisi Kasulu, akiwa katika ziara ya kukagua miradi inayotekelezwa chini ya Mpango wa Pamoja Kigoma (KJP).

Mkuu wa Mkoa Kigoma Balozi Simon Sirro akipata maelezo wakati wa ziara yake Kasulu, Picha na tovuti ya Mkoa Kigoma

Balozi Sirro amesena anasikitishwa na tabia iliyojengeka miongoni  mwa wakazi  ya kutokuwa tayari kutoa ushahidi kwenye vyombo vya sheria ikiwemo Jeshi la Polisi ili wanaohusika na vitendo hivyo waweze kuchululiwa hatua badala yake matukio  hayo yamekuwa yakimalizwa kijamii.

Amesema pamoja na uwepo wa changamoto hiyo ili kukabiliana na tatizo hilo katika hatua za awali, jamii inatakiwa kudumisha malezi bora na yenye maadili  kwa watoto hali itakayopunguza matukio ya ukatili.

Aidha amewataka watendaji katika madawati hayo kuhakikisha wanatekeleza wajibu wao kwa kuzingatia utu, misingi ya sheria pamoja na  kuzifanya ofizi hizo kuwa kimbilio kwa wanaokumbwa na kadhia zitokanazo na matukio ya hayo ya ukatili.

Mkuu wa Mkoa Kigoma Balozi Simon Sirro akisaini katika kitabu cha wageni wakati wa ziara yake Kasulu, Picha na tovuti ya Mkoa Kigoma

Kaimu Mkuu wa Dawati  la Jinsia na watoto Wilayani Kasulu Mkoani Kigoma Sperius Rweyemamu ameishukuru Serikali kwa kufanikisha uwepo wa dawati hilo kupitia ufadhili wa shirika la umoja wa mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF), kufuatia kukithiri kwa vitendo vya ubakaji, vipigo, ulawiti,  na migogoro ya kifamilia wilayani humo.

Sperius amezitaja changamoto zinazokinzana na juhudi za dawati hilo wilayani Kasulu kuwa ni wananchi kutoa taarifa za matukio nje ya saa 72, suluhu za makosa zinazotakiwa kupatikana kisheria kuamuliwa kijamii pamoja na mashahidi kuogopa kutoa taarifa za matukio hayo kwa visingizio vya kukosa nauli, muda au kudai malipo kutoka kwa ndugu au waathirika wa matukio ya ukatili.

Ameendelea kusisitiza kuwa, uwepo wa kundi kubwa la watoto wasio chini ya malezi ya wazazi au ndugu, kunachangia kuendelea kuwepo kwa matukio hayo katika jamii wilayani Kasulu.