Joy FM
Joy FM
2 July 2026, 11:01

Utoaji wa mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani na Halmashauri ni moja ya mikakati ya Serikali ya kuwawezesha wananchi kiuchumi, hususan wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ili kusaidia kuendeleza na kupanua shughuli za uzalishaji na biashara, jambo linalochangia kuongeza kipato na kuboresha maisha yao
Na Hagai Ruyagila
Halmashauri ya Mji Kasulu mkoani Kigoma imetoa mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa robo ya nne ya mwaka wa fedha 2025/2026 yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 261 kwa vikundi 24 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuwawezesha wananchi kiuchumi.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi hundi ya mkopo huo, mgeni rasmi ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Kasulu Mjini, Profesa Joyce Ndalichako, amewataka wanufaika kutumia fedha hizo kwa malengo yaliyokusudiwa ili ziwe chachu ya maendeleo ya kiuchumi, kuongeza kipato chao na kuhakikisha wanafanya marejesho kwa wakati kwa mujibu wa masharti ya mkopo.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Kasulu, Mheshimiwa Ayubu Ngalaba, ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Kigondo, amewasisitiza wanufaika kuwa waaminifu katika matumizi ya mikopo hiyo, kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zote za utoaji na urejeshaji wa mikopo ili kuwapa fursa wananchi wengine kunufaika.
Akisoma taarifa ya utekelezaji wa mpango huo, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kasulu ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Nurfus Aziz Ndee, amesema halmashauri imefanikiwa kutoa mikopo hiyo kwa vikundi 24 vinavyoundwa na wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, ikiwa ni utekelezaji wa takwa la kutenga asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa ajili ya makundi hayo.

Baadhi ya wanufaika wa mikopo hiyo wameahidi kutumia fedha hizo ipasavyo katika shughuli za uzalishaji na biashara ili kuinua uchumi wao, kuboresha maisha ya familia zao na kurejesha mikopo kwa wakati.
