Joy FM

POSTA yaboresha utoaji wa huduma za usafirishaji Kigoma

12 August 2026, 16:51

Mkurugenzi wa Masoko na Mauzo wa Shirika la Posta, Ferdinand Kabyemela , Picha na Lucas Hoha

Wafanyabiashara na wananchi Mkoani Kigoma wametakiwa kutumia fursa ya huduma ya EMS ya Posta Tanzania kusafirisha mizigo na bidhaa kwenda mataifa mbalimbali duniani, ikiwemo Marekani, ili kukuza biashara na kuongeza kipato

Na Lucas Hoha

Shirika la Posta Tanzania limesema limeanza kufanya maboresho makubwa katika utoaji huduma ya kusafirisha vifurushi nje ya nchi, ikiwemo kutumia mtandao wa kompyuta kumuwezesha mteja kufuatilia mzigo wake tangu ulipokabidhiwa kwa shirika hilo hadi ulipo kwa wakati huo.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Kigoma, Mkurugenzi wa Masoko na Mauzo wa Shirika la Posta, Ferdinand Kabyemela amesema mpango huo unalenga kuondoa dhana iliyojenga kwa Watanzania wengi kwamba mizigo inayosafirishwa na shirika hilo inachukua muda mrefu kufika na wakati mwingine kupotea.

Amesema ili kukabiliana na hali hiyo, shirika limeanza mkakati wa kuhakikisha vifurushi vinavyotumwa vinachukua siku chache tangu vilipokabidhiwa kwao, hadi kufika vinapotakiwa kwenda na kwamba hiyo itajenga imani na kuwafanya wateja kurudisha uzalendo katika kutumia huduma za shirika hilo.

Naye Mkurugenzi wa Huduma za Posta Tanzania, Arubee Ngaruka, amesema wameamua kuimarisha matumizi ya EMS kwa kuwa ni mfumo wa kisasa unaolenga kurahisisha usafirishaji wa mizigo kwa wananchi.

Amesema wananchi wa Kigoma wana nafasi kubwa ya kunufaika na huduma hiyo, kutokana na wafanyabiashara wa mkoa huo kuwa wadau muhimu wa Posta kupitia usafirishaji wa mazao yanayotokana na shughuli za uvuvi.

Baadhi ya watumishi wa Posta, Picha na Lucas Hoha

Naye Meneja wa Posta Mkoa wa Kigoma, Ndagije Patrick Chobaliko, amesema kampeni ya EMS imeanza kuleta matokeo chanya mkoani humo, baada ya wafanyabiashara kupata fursa zaidi ya kusafirisha bidhaa zao kwenda masoko ya kimataifa.

Amesema awali kulikuwa na changamoto kwa wafanyabiashara waliokuwa wakihitaji kusafirisha bidhaa mbalimbali, hasa samaki kwenda Marekani, lakini maboresho ya huduma hiyo yamefungua fursa mpya kwa wafanyabiashara wa Kigoma.

Chobaliko amewahimiza wafanyabiashara na wananchi kutumia huduma za Posta katika kusafirisha bidhaa zao, akieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kuwaunganisha na masoko ya nje na kuchangia katika kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja, Mkoa wa Kigoma na Taifa kwa ujumla.