Joy FM

Madiwani waagiza ununuliwe mtambo kuchonga barabara Kigoma

5 May 2026, 13:52

Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, Picha na Ofisi ya mawasiliano Kigoma Manispaa

Kutokana na barabara nyingi za Manispaa ya Kigoma Ujiji kuharibika kutokana na mvua, Madiwani katika manispaa hiyo wameagiza ofisi ya mkurugenzi kununua mtambo kwa ajili ya ukarabati wa barabara hizo.

Na Mwandishi wetu

Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji inapanga kununua mtambo wa kuchonga barabara utakaosaidia halmashauri hiyo kukarabati barabara za mtaani ili ziweze kupitika kwa urahisi muda wote iwe masika au kiangazi na kuwezesha shughuli za kiuchumi na kjamii kuendelea bila kikwazo.

Uamuzi wa kununua mtambo huo umefikiwa katika kikao cha robo ya tatu ya Januari –Machi 2026 cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji, ukilenga kuifanya halmashauri hiyo kuwa na uwezo wa kukarabati barabara zake yenyewe na kutatua matatizo ya miundombinu ya barabara katika mji wa Kigoma.

Awali wakichangia suala hilo baadhi ya madiwani akiwemo Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kigoma Ujiji Musa Maulid, wamesema hali ya barabara ndani ya Manispaa hiyo ni mbaya kwa kiwango ambacho kinatia aibu, hivyo ununuzi wa mtambo huo ni suala ambalo linatakiwa kupewa kipaumbele muhimu.

Akihitimisha hoja hiyo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji, Kisena Mabuba, amesema kwa sasa halmashauri haina pesa kwa ajili ya kununua mtambo huo hivyo inategemea fedha zitakazotokana na malipo ya fidia ya ardhi na majengo kutoka kwenye mradi wa Reli ya Kisasa SGR.