Joy FM

DC Kigoma asisitiza utatuzi wa migogoro ya ardhi kisheria

15 August 2026, 12:58

Mkuu wa Wilaya Kigoma akiwa anazungumza na wananchi wakati wa zoezi la kusikiliza na kutatua changamoto za migogoro ya ardhi, Picha na Mwandishi wetu

Ardhi ni rasilimali muhimu katika maisha ya binadamu kwa sababu hutumika kwa makazi, kilimo, biashara, uwekezaji pamoja na ujenzi wa miundombinu ya huduma za kijamii, hata hivyo, pamoja na umuhimu wake, migogoro ya ardhi imeendelea kuwa changamoto katika jamii nyingi ambayo hujitokeza kati ya wananchi wenyewe, familia, majirani, wawekezaji, wafugaji na wakulima, pamoja na wananchi na mamlaka mbalimbali

Na Mwandishi wetu

Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Dkt. Rashid Chuachua, ameendelea kupokea, kusikiliza na kutatua migogoro ya ardhi inayowakabili wananchi, huku akisisitiza umuhimu wa kufuata taratibu na sheria katika umiliki na matumizi ya ardhi.

Mkuu wa Wilaya Kigoma akiwa anazungumza na wananchi wakati wa zoezi la kusikiliza na kutatua changamoto za migogoro ya ardhi, Picha na Mwandishi wetu

Dkt. Chuachua amekuwa akipokea wananchi ofisini kwake kwa ajili ya kusikiliza kero na malalamiko mbalimbali yanayohusu ardhi, sambamba na kufanya ziara katika maeneo yenye migogoro ili kupata uhalisia wa changamoto hizo.

Alhamisi, Agosti 12, Mkuu wa Wilaya Dkt. Chuachua aliwasikiliza wananchi waliowasilisha migogoro mbalimbali inayohusiana na ardhi katika ofisi yake ambapo baada ya kusikiliza malalamiko hayo, alifanya ziara katika baadhi ya maeneo yaliyotajwa kuwa na migogoro kwa lengo la kujionea hali halisi na kuzungumza na wahusika.

Miongoni mwa maeneo aliyotembelea ni eneo lililopo Mtaa wa Msufini, Kata ya Businde, Manispaa ya Kigoma Ujiji, ambalo limekuwa likigombaniwa na baadhi ya wananchi wa eneo hilo.

Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa wakati wa ziara hiyo, mmoja wa wakazi wa eneo hilo, Tawfiq Haruna, anadai kuwa eneo hilo alilirithi kutoka kwa mzazi wake. Aidha, wananchi walieleza kuwa eneo hilo limekuwa likiuziwa watu kwa kushirikiana na mwenyekiti wa mtaa.

Dkt. Chuachua alifika Kata ya Businde kufuatia malalamiko yaliyowasilishwa na wananchi wakiongozwa na Diwani wa Kata ya Businde, Masoud, kuhusu uwepo wa maeneo mbalimbali yanayodaiwa kuuzwa na watu waliojimilikisha maeneo hayo bila kufuata taratibu.

Wananchi walieleza kuwa hali hiyo imechangia kupungua kwa maeneo yanayoweza kutumika kwa ajili ya kujenga na kuendeleza miundombinu ya huduma za kijamii katika kata hiyo.

Katika ziara hiyo, Mkuu wa Wilaya alikutana na wajumbe wa Serikali ya Mtaa, wazee, wananchi pamoja na pande zinazohusika katika mgogoro huo.

Baada ya kusikiliza maelezo kutoka pande mbalimbali, Dkt. Chuachua alitoa maelekezo yenye mwelekeo wa kutatua mgogoro huo kwa kuzingatia sheria, taratibu na maslahi ya wananchi.

Hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali katika kuhakikisha migogoro ya ardhi inatatuliwa kwa wakati, haki na kwa kuzingatia taratibu za kisheria, huku maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya huduma za kijamii yakilindwa dhidi ya uvamizi na uuzwaji usio halali.