Joy FM
Joy FM
29 June 2026, 14:35

Serikali imeendelea kutekeleza mpango wa utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kupitia Halmashauri mbalimbali nchini kwa lengo la kuwawezesha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kujikwamua kiuchumi.
Na Emmanuel Kamangu
Jumla ya zaidi ya shilingi milioni 600 zimetolewa na Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, mkoani Kigoma, kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kupitia mpango wa mikopo ya asilimia 10, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuwawezesha wananchi kujikwamua kiuchumi.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma katika hafla ya utoaji wa mikopo kwa robo ya tatu na ya nne ya mwaka wa fedha 2025/2026, Katibu Tawala wa Mkoa, CPSP Hassan Rugwa, amewataka wanufaika kutumia mikopo hiyo kwa malengo yaliyokusudiwa ili iweze kuleta tija na kuboresha maisha yao.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Kanal Isack Mwakisu, amesema ushirikiano na umoja uliopo miongoni mwa watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu ni miongoni mwa sababu zinazowezesha utoaji bora wa huduma kwa wananchi, ikiwemo usimamizi na utoaji wa mikopo ya asilimia 10.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, CPA Fransis Kafuku, amesema elimu inayoendelea kutolewa kwa wanufaika wa mikopo hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa kuimarika kwa urejeshaji wa fedha kwa wakati, hali inayowezesha vikundi vingine kunufaika na mfuko huo.
Baadhi ya wanufaika wa mikopo hiyo wameishukuru Serikali kwa kuendelea kuweka mazingira rafiki ya kuwawezesha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kupitia mikopo ya asilimia 10, wakisema imewapa fursa ya kuanzisha na kuendeleza shughuli za kiuchumi.
Katika mgao huo wa mikopo, fedha zimetumika kuwezesha ununuzi wa pikipiki 13, seti tatu za mashine za kusaga, pamoja na mashine moja ya kuchakata nafaka na vyereheni.