Joy FM

Kituo cha afya chazinduliwa Uvinza

4 June 2026, 12:37

Muonekano wa kituo cha afya Sunuka Wilaya ya Uvinza, Picha na Mwandishi wetu

Huduma za afya karibu na maeneo ya wananchi husaidia kupunguza gharama na muda wa kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya mbali za maeneo.

Na Mwandishi wetu

Wananchi wa Kata ya Sunuka na maeneo jirani wamepata ahueni baada ya kuzinduliwa rasmi kituo cha afya Sunuka, mradi uliogharimu takribani shilingi milioni 400. Kituo hicho kinatarajiwa kuboresha upatikanaji wa huduma za afya na kupunguza changamoto ya kusafiri umbali mrefu kufuata matibabu.

Akizungumza katika mkutano wa wananchi wakati wa uzinduzi huo, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Dkt. Biseko Maira, amesema kuwa kukamilika kwa kituo hicho ni utekelezaji wa dhamira ya Serikali ya kusogeza huduma muhimu karibu na wananchi na kuboresha ustawi wa jamii.

Wananchi wa Kata ya Sunuka wakiwa kwenye mkutano wa hadhara, Picha na Mwandishi wetu

“Kwa siku ya leo tumefanikiwa kumfanyia upasuaji mama mjamzito mmoja na anaendelea vizuri sambamba na mtoto wake” amesema Dr. Biseko

Watoa huduma wakitoa huduma kwa mgonjwa kituo cha afya Sunuka Uvinza, Picha na Mwandishi wetu

Wananchi wa Sunuka na kata jirani wameishukuru Serikali kwa kusikiliza kilio chao cha muda mrefu kilichodumu kwa takribani miaka minne, wakieleza kuwa ujio wa kituo hicho utarahisisha upatikanaji wa huduma za afya na kuokoa muda pamoja na gharama walizokuwa wakitumia kufuata matibabu katika maeneo ya mbali.