Joy FM

Diwani alia wananchi kukosa bima ya afya bure Kasulu

29 April 2026, 13:27

Diwani wa kata ya Heru Ushingo Ezrom Ntegeye, Picha na Hagai Ruyagila

Serikali katika Halmashauri ya Wilaya Kasulu Mkoani Kigoma imesema inaendelea kushirikiana ili kuhakikisha wanawapatia bima wananchi wote

Na Hagai Ruyagila

Diwani wa Kata ya Heru Ushingo Mh Ezrom Ntegeye kutoka Halmashauri ya wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma ameomba kupatiwa ufafanuzi wa kina kuhusu sababu zilizosababisha baadhi ya wanufaika wa kaya masikini katika kata hiyo majina yao kukosekana wakati wa kugawa bima za afya bila malipo zinazotolewa na Serikali, jambo ambalo limeibua hisia mchanganyiko miongoni mwa wananchi.

Mh Ntegeye. Amesema kuna idadi ya wananchi waliotambuliwa kuwa ni kaya masikini, lakini majina yao hayajajumuishwa katika orodha ya wanufaika wa mpango huo, hali inayowanyima fursa ya kupata huduma za afya bila gharama. Amesisitiza umuhimu wa serikali kutoa maelezo ya wazi ili kuondoa sintofahamu na kuhakikisha haki inatendeka kwa walengwa wote.

Diwani wa kata ya Heru Ushingo Ezrom Ntegeye, Picha na Hagai Ruyagila

Ameongeza kuwa ufafanuzi huo utasaidia pia kubaini changamoto zilizopo katika mchakato wa utambuzi na usajili wa wanufaika, pamoja na kuweka mikakati ya kuzitatua ili kuhakikisha huduma hiyo inawafikia walengwa waliokusudiwa.

Sauti ya Diwani wa kata ya Heru Ushingo Ezrom Ntegeye

Akijibu swali hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, CPA Francis Kafuku, amesema kuhusu changamoto hiyo, halmashauri inaendelea kufanya mawasiliano na watu wa bima ya afya ili kuondoa ukanganyiko huo uliojitokeza.

Sauti ya CPA Francis Kafuku
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, CPA Francis Kafuku, Picha na Hagai Ruyagila