Joy FM
Joy FM
7 July 2025, 12:19

Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Wesern Tanganyika amewataka wachungaji kuwatumikia kwa upendo.
Na Hagai Ruyagila
Wachungaji na viongozi wa Kanisa la Anglikana, Dayosisi ya Western Tanganyika (DWT), wametakiwa kuachana na roho ya chuki na migawanyiko miongoni mwao, badala yake kumtumikia Mungu kwa furaha, upendo na bidii, huku wakichangia katika maendeleo ya kiuchumi katika maeneo yao ya utumishi ili huduma ya Mungu iendelee kusonga mbele kwa mafanikio..
Wito huo umetolewa na Askofu wa Dayosisi hiyo, Mhashamu Emmanuel Bwatta, wakati akihitimisha mkutano mkubwa wa injili uliofanyika katika makao makuu ya Kanda ya Ziwa, eneo la Kidahwe, mkoani Kigoma.
Katika hotuba yake, Askofu Bwatta amesisitiza kuwa mafanikio ya huduma ya Mungu yanategemea sana moyo wa kujitolea na mshikamano miongoni mwa viongozi wa kanisa na waumini, akibainisha kuwa chuki, fitina na ubinafsi vinaweza kudhoofisha kazi ya Mungu.
Mkurugenzi wa kanisa la Anglikana Kanda ya Kasulu Mjini, Mchungaji Canon Laurent Magogwa amesisitiza kufanyakazi ya Mungu kwa furaha na moyo wa shukrani, huku akisema kuwa kanisa haliwezi kupiga hatua bila mshikamano pia amewaomba waumini kuwa tayari kutoa sadaka ili kuchangia maendeleo ya kanisa.

Baadhi ya Wachungaji wa kanisa hilo akiwemo Mchungaji Yohana Bhitona, Anderson Bilasa na Shemasi Abia Mpuzu wamesema wamepokea maelekezo hayo ambayo yatakwenda kuwasaidia kuboresha huduma zao kwa bidii na ufanisi zaidi katika maeneo yao ya utumishi wao.
Mkutano huo wa injili umehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kanisa la Anglikana Dayosisi ya Western Tanganyika, wachungaji, na waumini kutoka maeneo tofauti ya mkoa wa Kigoma, lengo kuu ni kuimarisha kiroho waumini pamoja na kutoa hamasa ya kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii na dayosisi hiyo.
