Joy FM
Joy FM
15 July 2026, 12:54

Biashara ni nguzo muhimu ya maendeleo ya wananchi na uchumi wa taifa. Katika Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza, Mkoa wa Kigoma, wanawake wengi hujishughulisha na biashara ya chumvi kama njia ya kujipatia kipato na kukidhi mahitaji ya familia zao. Hata hivyo, changamoto ya ukosefu wa masoko ya uhakika imeendelea kuathiri biashara hiyo, jambo linalopunguza mapato yao na kudhoofisha ustawi wa familia
Na Timotheo Leonard
Wanawake wanaofanya biashara ya chumvi katika Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza Mkoani Kigoma, wameiomba Serikali kuwatafutia masoko ya uhakika baada ya mauzo yao kushuka kutoka mifuko minne hadi mmoja kwa siku.
Wakizungumza na Radio Joy Fm katika Kijiji cha Ruchugi, wanawake hao wamesema changamoto hiyo ilianza baada ya kuondolewa katika eneo lao la awali la biashara.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Ruchugi Ramadhani Kayungilo ameshauri wafanyabiashara hao kuongeza thamani ya chumvi kupitia vifungashio bora na kujiunga katika vikundi vya kiuchumi.

Naye mwezeshaji wa vikundi vya kuweka na kukopa, Juma Iddi amebainisha kuwa wanaendelea kuwajengea uwezo wafanyabiashara hao kwa kuwapatia vifungashio vinavyoongeza thamani ya bidhaa.
Kwa upande wake, Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza, Getruda Sipocha, amesisitiza kuwa halmashauri inaendelea kutoa mafunzo ya urasimishaji wa biashara na kuongeza thamani ya bidhaa ili kuwasaidia kupata masoko.