Joy FM

Wahasibu wajadili ufungaji wa hesabu za mwaka 2025/ 2026 Kakonko

18 May 2026, 16:31

Wahasibu wa Mkoa wa Kigoma wakiwa katika kikao kazi maalumu cha maandalizi ya ufungaji wa hesabu za mwaka wa fedha 2025/2026, Picha na Ofisi ya Mawasiliano Kakonko

Ufungaji wa hesabu za mwaka wa fedha ni hatua muhimu katika usimamizi wa fedha za taasisi mbalimbali za serikali na binafsi na una umuhimu mkubwa kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii

Na Mwandishi wetu

Wahasibu kutoka halmashauri zote 8 za Mkoa wa Kigoma wamekutana Wilayani Kakonko katika kikao kazi maalumu cha maandalizi ya ufungaji wa hesabu za mwaka wa fedha 2025/2026, kwa lengo la kuimarisha usimamizi wa fedha za umma na kuhakikisha taarifa za kifedha zinaandaliwa kwa wakati na kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo ya Serikali.

Kikao hicho kimefanyika leo Mei 18, 2026 ambapo kimewakutanisha wataalamu wa fedha na wahasibu kutoka halmashauri mbalimbali za mkoa wa Kigoma, kimejikita katika kujadili mbinu bora za uandaaji wa hesabu za mwisho wa mwaka, utunzaji sahihi wa nyaraka za kifedha pamoja na kuondoa changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa zoezi la ufungaji wa hesabu.

Akifungua kikao hicho kwa niaba ya Katibu Tawala wa mkoa wa Kigoma ambaye alialikwa kuwa mgeni rasmi, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko, Ndaki Stephano Mhuli amesisitiza umuhimu wa uwajibikaji, nidhamu ya matumizi ya fedha za umma pamoja na kuzingatia viwango vya kitaaluma katika uandaaji wa taarifa za kifedha ili kuongeza ufanisi na uwazi katika Halmashauri.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko, Ndaki Stephano Mhuli, Picha na Ofisi ya Mawasiliano Kakonko

Aidha, wahasibu hao wamekumbushwa kuhakikisha mifumo ya kifedha inatumika ipasavyo na taarifa zote muhimu zinawasilishwa kwa wakati ili kuwezesha ukaguzi wa hesabu kufanyika kwa ufanisi.

Washiriki wa kikao hicho wameeleza kuwa mafunzo na mijadala inayotolewa itasaidia kuongeza uelewa wa pamoja na kuimarisha ushirikiano miongoni mwa wahasibu wa halmashauri za Mkoa wa Kigoma katika kusimamia fedha za Serikali kwa ufanisi zaidi.

Kikao kazi hicho cha siku tano kilichoanza leo kinatarajiwa kuhitimishwa siku ya Ijumaa Mei 22, 2026 kwa kutoa maazimio na mikakati mbalimbali itakayosaidia kuboresha mchakato wa ufungaji wa hesabu za mwaka wa fedha 2025/2026 katika halmashauri zote za Mkoa wa Kigoma.