Joy FM

UNDP, SIDO zawainua wafugaji samaki Kibondo

11 May 2026, 13:18

Miongoni mwa wanachama wa kikundi cha ufugaji samaki akiweka chakula kwenye bwawa la samaki, Picha na Mwandishi wetu

Ufugaji wa samaki kwenye vizimba ni njia muhimu ya kuwawezesha vijana kiuchumi, kuongeza ajira, na kuchangia maendeleo ya jamii na taifa.

Na Mwandishi wetu

Baadhi ya wafugaji wa samaki Wilayani Kibondo Mkoani Kigoma wameiomba jamii Wilayani humo kuendelea kuthamini na kuunga mkono uwekezaji unaofanywa kwenye maeneo yao ili kukuza uchumi wa wazawa na halmashauri kwa ujumla.

Halmashauri kupitia idara ya maendeleo ya jamii imekuwa ikihamasisha vijana kuunda vikundi na kuanzisha miradi ya maendeleo ili waweze kutambuliwa na kuendelezwa kupitia mikopo ya asilimia 4 kwa vijana, 4 kwa wanawake na 2 kwa watu wenye ulemavu.

Miongoni mwa wanachama wa kikundi cha ufugaji samaki akiweka chakula kwenye bwawa la samaki, Picha na Mwandishi wetu

Baadhi ya wafugaji wa samaki kutoka kikundi cha Bondeni Fish Farmingi kilichopo Kilemba Kibondo ambao ni Bw. Alex Ntenderi na Bw. Braison Juma wamesema kiu yao ni kuona mazao ya samaki yakiwa utambulisho mkubwa kwa wilaya ya Kibondo kwani samaki wanaofugwa kwenye mabwawa yao hayana utofauti na wanaotoka kwenye maeneo mengine hasa ziwa vikitoria na mito mingine kwa maana ya Kambare.

Sauti ya Mfugaji wa samaki

Bw. Alex Ntenderi anasema hadi kufikia mafanikio hayo ni juhudi kubwa ambazo wadau wamezifanya ikiwemo halmashauri ya wilaya ya Kibondo, Shirika la UNDP pamoja na shirika la kuhudumia viwanda Vidogo SIDO na kwamba bado wanahitaji uungwaji mkono hasa katika changamoto ya mashine ya kuzalisha vyakula vya samaki ambayo inagharimu zaidi ya shilingi milioni 12.

Muonekano wa samaki kwenye bawa la kufugia samaki Kibondo, Picha na Mwandishi wetu