Joy FM

TAKUKURU yawafungulia mashitaka viongozi wa ushirika kwa udanganyifu Kasulu

14 July 2026, 13:03

Muonekano wa ofisi ya Taasisi ya kuzuia na Kupambana na Rushwa Kasulu, Picha na Mtandao

Kiongozi anapopewa jukumu la kusimamia rasilimali za wanachama, anapaswa kufanya hivyo kwa uwazi na uaminifu na fedha zinazotokana na shughuli za chama zinapaswa kugawanywa kwa haki kulingana na taratibu zilizowekwa

Na Mwandishi wetu

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Takukuru Wilaya ya Kasulu imewafungulia mashitaka viongozi wanne wa chama cha ushirika AMKENI kilichopo kata ya kurugongo halmashauri ya Wilaya ya kasulu mkoani Kigoma kwa kosa la udanganyifu wa fedha za chama hicho. 

Akizungumza na waandishi wa Habari jana julai 13 katika mahakama ya wilaya ya kasulu mwendesha mashitaka wa serikali kutoka taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa TAKUKURU wilaya ya Kasulu Davis Junior amesema miongoni mwa washitakiwa hao ni Barton Cosmas Rushikigwa, Reuben Kazala Kivyoma na Dominiko Lameck Lusibo wote wakiwa viongozi wa chama cha Ushirika AMKENI kata ya Kurugongo.

Aidha amesema kuwa washitakiwa hao wameshitakiwa kwa kosa la kufanya udanganyifu wa kujizidishia fedha za chama hicho walizotakiwa kugawana baada ya kuuza tumbaku hali iliyopelekea baadhi ya wanachama wenzao kukosa haki ya kunufaika na fedha hizo na wengine kupata kiwango kidogo cha malipo.

Sauti ya Mwendesha mashitaka

Kesi hizo zitarejea tena mahakamani tarehe 20 na 21 ya mwezi huu wa Julai 2026 kwa ajili ya watuhumiwa kusomewa hoja za awali na kwa upande wa jamhuri wao wanasema ushahidi umeshakamilika.