Joy FM

AU kujenga na kuimarisha daraja kwa nchi zilizositishwa uanachama

21 April 2026, 09:19

Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye kwenye picha ya pamoja na Rais Ibrahim Traore, Picha na Bukuru Elias

Hatua hiyo inaweza kusaidia kurejesha utulivu wa kisiasa kwa kuzijenga upya kidiplomasia na inaweza kusaidia nchi hizo kurudi kwenye mfumo wa utawala wa sheria, jambo ambalo linaimarisha amani katika kanda

Na Bukuru Elias

Ofisi ya Rais wa Burundi imesema kuwa mazungumzo kati ya Evariste Ndayishimiye na Ibrahim Traoré yamejikita katika kutafuta njia za kujenga na kuimarisha daraja kati ya Umoja wa Afrika na muungano wa nchi za Sahel zilizositishwa uanachama wake.

Awali, ofisi ya Evariste Ndayishimiye ilikuwa imetangaza kuwa alisafiri kwenda Ouagadougou kwa ziara ya kikazi na kirafiki. Ziara hiyo ina uzito mkubwa kwani kwa sasa yeye ndiye mwenyekiti wa Umoja wa Afrika mwaka huu.

Mazungumzo hayo yanakuja wakati ambapo uhusiano kati ya Umoja wa Afrika na nchi za Burkina Faso, Guinea na Mali umeendelea kuwa na mvutano kufuatia mapinduzi ya kijeshi yaliyotokea kati ya mwaka 2021 na 2022 ambapo umoja huo uliamua kuzisimamisha nchi hizo kulingana na taratibu zake.

Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye kwenye picha ya pamoja na Rais Ibrahim Traore, Picha na Bukuru Elias

Licha ya jitihada za kurejesha mazungumzo na ushirikiano, baraza la amani na Usalama la umoja wa Afrika hivi karibuni lilisema bado kuna changamoto kubwa katika kurejesha ushirikiano kamili na mamlaka ya umoja huo katika nchi hizo.

Katika ripoti yake ya mwezi uliopita, Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika lilieleza kuwa licha ya kuwepo kwa mazungumzo ya faragha, bado kuna changamoto kubwa kwa umoja huo kurejesha ushawishi na nafasi yake katika nchi zilizokumbwa na mapinduzi ya kijeshi.

Rais wa Burundi Evariste Ndayishiye akisaliiana na Rais Ibrahim Traore, Picha na Bukuru Daniel

Hatua hii inaonyesha juhudi zinazoendelea za kutafuta suluhisho la pamoja katika eneo la Sahel, wakati changamoto za usalama na utawala zikiendelea kuathiri ukanda huo,Burkina Faso, Guinea na Mali zikiwa zimeunda muungano wa nchi tatu za Afrika Magharibi unaoitwa Confédération des États du Sahel kwa kifaransa, unaoongozwa na Ibrahim Traoré.

Ziara hii inafanyika baada ya jitihada za Umoja wa Afrika za kuimarisha tena uhusiano na baadhi ya nchi za Afrika Magharibi zilizofungiwa kushiriki katika umoja huo kufuatia mapinduzi ya kijeshi yaliyotokea katika miaka ya hivi karibuni.

Katika siku za hivi karibuni, Rais wa Burkina Faso, Ibrahim Traoré, alizua mjadala baada ya kusema kuwa nchi yake haihitaji demokrasia kwa sababu huua, kauli iliyochukuliwa kwa mitazamo tofauti na wachambuzi wa siasa.

Ziara ya Evariste Ndayishimiye nchini Burkina Faso inakuja kufuatia juhudi za Umoja wa Afrika za kurekebisha na kuimarisha tena uhusiano na nchi hizo, licha ya kuwepo kwa tofauti za kisiasa na kiutawala.