Joy FM

UN Women kusaidia wanawake na vijana 3500 Kigoma

13 June 2026, 12:55

Mwakilishi wa UN Women akiwa kwenye picha na RAS Kigoma mara baada ya uzinduzi mradi, Picha na Mwandishi wetu

Mabadiliko ya tabianchi yamekuwa yakiathiri sehemu kubwa ya ustawi wa watu wenye ulemavu, wanawake na vijana katika shughuli mbalinbali za uzalishaji mali.

Na Mwandishi wetu

Shirika la Umoja wa Mataifa la Usawa wa Jinsia na Uwezeshaji wa Wanawake (UN Women) linatarajia kuwasaidia takriban wanawake na vijana 3500 walioathirika na mabadiliko ya tabia nchi mkoani Kigoma.

Zabibu Mkamba Mwakilishi wa Katibu Tawala mkoa Kigoma, Picha na Mwandishi wetu

Mwakilishi wa UN Women nchini Tanzania, Katherine Gifford, wakati wa uzinduzi wa mradi wa kuimarisha maandalizi ya kukabiliana na majanga na ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi kwa kuzingatia jinsia unaotekelezwa na UN WOMEN kwa ufadhili wa serikali ya japan.

Katherine amesisitiza umuhimu wa kuwaweka wanawake na vijana katika kitovu cha juhudi za kujenga ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na maandalizi ya kukabiliana na majanga Ambapo Mradi unatarajiwa kuwafikia moja kwa moja watu 700 wakiwemo wanawake 570 na kunufaisha kwa njia isiyo ya moja kwa moja takribani watu 3,500.

Catherine Gifford Mwakilishi Mkazi wa UN Women Tanzania

Mwakilishi huyo wa UN Women alisema kuwa Mabadiliko ya tabianchi na majanga hayaathiri watu wote kwa kiwango sawa bali Wanawake na wasichana mara nyingi hukabiliwa na hatari kubwa zaidi, lakini pia ndio wanaoongoza katika kujenga ustahimilivu na kuendesha juhudi za kupona baada ya majanga.

Awali Katibu Tawala wa mkoa Kigoma, Hassan Rugwa alisema kuwa wasichana,watu wenye ulemavu na makundi maalum wamekuwa wahanga wakubwa wa mabadiliko ya tabia nchi yanayotokea mkoani humo na kuathiri maisha yao na shughuli zao za kiuchumi.

Katika hotuba iliyotolewa kwa niaba yake na Katibu Tawala Msaidizi huduma utumishi ofisi ya Mkuu wa mkoa Kigoma, Zabibu Mkamba alisema kuwa mkoa Kigoma umekuwa ukikabiliwa na changamoto za mabadiliko ya tabia nchi ambayo yamekuchangia kuvuruga shughuli za kilimo, kupotea kwa mali na kuathiri shughuli za kujiingizia kipato kwa makundi hayo.

Pamoja na hilo Rugwa amesema kuwa kuzinduliwa kwa mradi huo siyo mwanzo wa kujenga ustahimilivu kwa changamoto za tabia nchi bali serikali na wadau wamekuwa wakifanya shughuli za changamoto hizo kwa muda mrefu na kwamba mradi huo unaongeza chachu katika kujenga uwezo wa taasisi, uratibu na kuendeleza mifumo ya kupunguza hatari za majanga inayozingatia jinsia.