Joy FM
Joy FM
5 August 2026, 12:52

Kongamano hilo limeelezwa kuwa sehemu ya juhudi za Kanisa la PEFA kuwawezesha wanawake kwa kuwapa maarifa ya ujasiriamali, usimamizi wa fedha na mbinu za kujitegemea kiuchumi
Na Lucas Hoha
Wanawake wa Kanisa la Pentecostal Evangelistic Fellowship of Africa (PEFA) Mkoa wa Kigoma wamehimizwa kufanya kazi kwa bidii ili kujikwamua kiuchumi, huku wakipewa jukumu la kulea watoto katika maadili mema yatakayojenga kizazi kinachomcha Mungu na kulifaa Taifa.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Wanawake Taifa wa Kanisa la PEFA, Mchungaji Mathelesta Kifalu, wakati wa Kongamano la Wanawake wa PEFA Mkoa wa Kigoma lililofanyika kwa siku tatu. Kongamano hilo lililenga kuwajengea wanawake uwezo kupitia mafunzo ya ujasiriamali na mbinu mbalimbali za kujikwamua kutoka kwenye umasikini.
Mchungaji Kifalu amesema wanawake wana nafasi kubwa ya kuboresha uchumi wa familia na jamii kwa ujumla kupitia kazi na shughuli za uzalishaji. Pia amewataka kusimamia maadili na kupinga vitendo vinavyokwenda kinyume na mafundisho ya imani yao.
Kwa upande wake, Mwangalizi wa Kanisa la PEFA Wilaya ya Kigoma, Mchungaji Amani Yungi, amesema kanisa hilo linaendelea na kampeni maalumu ya kuwawezesha wanawake kiuchumi kwa lengo la kuwasaidia kujitegemea na kumtumikia Mungu pamoja na kulitumikia Taifa kwa ufanisi.

Baadhi ya wanawake walioshiriki kongamano hilo wamesema mafunzo waliyopata yatawasaidia kuboresha maisha yao kwa kufanya kazi kwa bidii, kuanzisha shughuli za kujiongezea kipato na kushirikiana na waume zao katika kuimarisha uchumi wa familia.