Joy FM

DC Kasulu aongoza maadhimisho miaka 20 ya Polisi jamii

1 September 2026, 15:54

Kamanda wa Polisi Kigoma akiwa na Mkuu wa Wilaya Kasulu kwenye kilele cha miaka 20 ya Polisi, Picha na Mwandishi wetu

Katika kuadhimisha miaka 20 ya Polisi jamii shughuli mbalimbali zimefanyika ikiwemo usafi wa mazingira katika maeneo mbalimbali huku Jeshi hilo likitoa wito kwa wananchi kushirikiana katika kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu

Na Mwandishi wetu

Mkuu wa Wilaya ya Kasulu Kanali Isaac Mwakisu ameongoza zoezi la usafi wa Mazingira katika Halmashauri hiyo akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Kigoma katika maadhimisho ya kilele cha miaka 20 ya Polisi Jamii ngazi ya Mkoa.

Akizungumza mara baada ya kushiriki usafi katika soko la Kumsenga lililopo wilayani humo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho hayo yaliyofanyika Agosti 29, 2026, Kanali Mwakisu amesema jamii inapaswa kuhakikisha mazingira yanakua safi wakati wote.

Mkuu wa Wilaya Kasulu akiwa katika maadhimisho ya Polisi jamii Kasulu, Picha na Mwandishi wetu

Amesema hatosita kuchukua hatua kali dhidi ya watakaopuuza zoezi hilo na kusababisha mrundikano wa uchafu katika maeneo ya makazi na yale ya kutolea huduma za jamii ikiwemo masoko.

Amesisistiza kuwa, kutokuzingatia usafi kunaweza sababisha maradhi ya mlipuko, hivyo kila mmoja anapaswa kutekeleza wajibu huo muhimu kwa ajili ya usalama wa Afya kwa wakazi.

SACP Philemon Makungu ambaye ni Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kigoma amesema sambamba na kuimarisha usalama, Jeshi hilo litaendelea kushiriki shughuli za kijamii ikiwemo kudumisha usafi wa Mazingira.

Kamanda wa Polisi akizungumza katika maadhimisho hayo, Picha na Mwandishi wetu

Aidha ametoa wito kwa wananchi kuendelea kushiriki shughuli za usafi pamoja na majukumu mengine yanayolenga kuimarisha ustawi wa jamii.

Mkuu wa Wilaya Kasulu akikabidhi zawadi, Picha na Mwandishi wetu

Maadhimisho ya Polisi Jamii kimkoa yamehitimishwa kwa bonanza la michezo mbalimbali lililofanyika katika uwanja wa Chuo cha Ualimu Kasulu yakiwa na kauli mbiu isemayo “ tushirikiane kuimarisha Amani, usalama na umoja wa taifa”