Joy FM
Joy FM
14 August 2026, 16:44

Shule za bweni ni taasisi ambazo wanafunzi huishi na kusoma katika mazingira ya shule kwa muda wote wa masomo kwa sababu hiyo, umeme ni huduma muhimu sana katika maisha yao ya kila siku
Na Hagai Ruyagila
Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Wilaya ya Kasulu Mkoani Kigoma limezitaka shule za sekondari zenye wanafunzi wanaoishi bweni kuboresha mifumo ya umeme pamoja na kuweka vifaa vya kuzimia moto, ili kukabiliana na majanga ya moto yanapojitokeza.
Akizungumza na walimu wa Shule za Sekondari Bogwe na Mwilanvya wakati wa mafunzo ya kinga na tahadhari dhidi ya majanga ya moto katika shule za bweni, Mkuu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Wilaya ya Kasulu, Mrakibu Msaidizi Antony Marwa, amesema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea walimu uelewa na uwezo wa kuchukua hatua sahihi wakati wa majanga ya moto.

Amesema shule za bweni zinapaswa kuhakikisha mifumo ya umeme inakaguliwa na kuboreshwa mara kwa mara ili kuzuia hitilafu zinazoweza kusababisha moto, huku akisisitiza umuhimu wa kuwepo kwa vifaa vya kuzimia moto katika mabweni ya wanafunzi.
Aidha, amezitaka taasisi za elimu kutoa taarifa kwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kabla ya kuanza ujenzi wa mabweni, ili kupata ushauri wa kitaalamu kuhusu hatua muhimu za kuzingatia katika ujenzi huo, ikiwemo uwekaji wa milango ya dharura kwa ajili ya kurahisisha uokoaji pindi moto unapotokea.

Kwa upande wao, baadhi ya walimu wa Shule ya Sekondari Bogwe wamesema mafunzo hayo yamewasaidia kuongeza uelewa na ujuzi wa kukabiliana na majanga ya moto, pamoja na kuwapa uwezo wa kuchukua hatua za haraka na sahihi katika kuwalinda wanafunzi na mali za shule.
