Joy FM
Joy FM
5 October 2026, 16:52
Wakati Dunia ikifanya maadhimisho ya siku ya Wazee Duniani, Baadhi ya Wazee katika Mkoa wa Kigoma wameomba jamii na Serikali kuendelea kuwajali na kuwalinda katika Nyanja zote za Maisha ikiwemo kupata matibabu ya uhakika na kwa wakati na watoto kuacha tabia ya kuwatelekeza wazazi wakati wao waliwalea na kuwapa mahitaji yote Mhimu ikiwemo kuwasomesha walipokuwa bado ni Watoto

Na Lucas Hoha
Akizungumza na Radio Joy Fm mara baada ya Maadhimisho hayo ambayo yamefanyika kwenye ukumbi wa Joy in The Harvest Kaimu Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Mkoa wa Kigoma Elias Kwengineza amesema licha ya Jitihada mbalimbali za Serikali katika kuboresha maisha ya Wazee bado sera za kuwalinda Wazee zinatakiwa kuangaliwa upya
Naye Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Kigoma Bi Epheta Msiga amesema Serikali wakishirikiana na wadau wa maendeleo wanaendelea kuweka mazingira rafiki ya Wazee kuishi, huku akisisitiza Wazazi wa kizazi cha sasa kutimiza wajibu kwa watoto ili baadae watoto wakishakuwa watu wazima nao waweze kuwatunza.
Kwa upande wake Mgeni rasmi kwenye Maadhimisho hayo Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma Bakari Tambwe amesema inasikitisha kuona baadhi ya Watoto wakiwatelekeza Wazazi wao na kujikuta wanalelewa kwenye vituo vya kulelea Wazee, huku akikemea tabia ya baadhi ya Wananchi kuwaona kama washirikina kitendo ambacho kinapelekea kufanyiwa ukatili.
Maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani Mwaka huu 2026 yamebebwa na Kauli mbiu isemayo Zama za Maisha marefu tuboreshe maisha kwa Wazee