Joy FM
Joy FM
26 November 2026, 20:45

Ujenzi wa barabara ya Shayo ni sehemu ya uboreshaji wa miundombinu ya usafiri katika Halmashauri ya Mji wa Kasulu ili ziweze kupitika hasa kipindi hiki cha mvua
Na Hagai Ruyagila
Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini TARURA Wilayani Kasulu mkoani Kigoma ameendelea na utekelezaji wa ujenzi wa barabara ya Shayo kwa kiwango cha lami kwa thamani ya shilingi milioni 545 hatua inayolenga kupunguza changamoto za usafiri na usafirishaji kwa watumiaji wa barabara hiyo.
Hayo yamebainishwa na Meneja wa (TARURA) Wilaya ya Kasulu, Mhandisi Peter Johnson, wakati akizungumza na vyombo vya habari ofisini kwake.Amesema ujenzi wa barabara hiyo umefikia asilimia 70, huku kazi inayoendelea kwa sasa ikiwa ni uwekaji wa makaravati.

Aidha, Mhandisi Johnson amesema ujenzi wa sehemu zilizobakia utaendelea kwa awamu nyingine kulingana na upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kuendelea na matengenezo ya Barabara hiyo.
Kwa upande wao, baadhi ya waendesha vyombo vya moto wamesema kukamilika kwa ujenzi wa barabara hiyo kutarahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji.
