Joy FM
Joy FM
18 November 2026, 11:33

Elimu kwa umma na ushirikiano wa wananchi vinaendelea kuwa sehemu muhimu katika juhudi za kukabiliana na vitendo vya rushwa katika maeneo ya biashara
Na Timotheo Leonard
Wanawake wachuuzi wa samaki katika Mwalo wa Kibirizi, Manispaa ya Kigoma Ujiji, wamesema vitendo vya rushwa ya ngono katika eneo hilo vimepungua, wakihusisha mabadiliko hayo na elimu iliyotolewa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Mkoa wa Kigoma.
Ni takribani miezi miwili sasa tangu TAKUKURU Mkoa wa Kigoma kutoa elimu kwa wanawake hao kuhusu madhara ya rushwa ya ngono, namna ya kukabiliana na vitendo hivyo pamoja na umuhimu wa kutoa taarifa kwa mamlaka husika.
Elimu hiyo ilitolewa kufuatia taarifa zilizowahi kuripotiwa kuhusu madai ya kuwepo kwa vitendo vya rushwa ya ngono katika Mwalo huo, ikiwemo taarifa zilizorushwa na Radio Joy FM.
Baada ya kupita kwa kipindi hicho, baadhi ya wanawake wachuuzi wa samaki wanasema wameanza kuona mabadiliko katika mazingira yao ya biashara, wakieleza kuwa vitendo hivyo vimepungua ikilinganishwa na hali iliyokuwepo awali.
Kwa upande wao, baadhi ya wavuvi katika Mwalo wa Kibirizi wamewataka wanawake kutumia mitaji waliyonayo kuendesha biashara zao badala ya kushawishika kuingia katika vitendo vya rushwa ya ngono ili kupata samaki.
Akizungumzia hali hiyo, Mwenyekiti wa Mtaa wa Kibirizi, Kudra Jafari, amesema kwa mtazamo wa uongozi wa eneo hilo, vitendo vya rushwa ya ngono vimepungua kufuatia wananchi kupatiwa elimu kuhusu madhara ya vitendo hivyo.
Naye Mkuu wa Dawati la Elimu kwa Umma TAKUKURU Mkoa wa Kigoma, Ibrahim Sadick, amesema taarifa wanazozipokea zinaonesha dalili za kupungua kwa vitendo hivyo.
Sadick amesisitiza kuwa TAKUKURU itaendelea kutoa elimu kwa wananchi ili kuongeza uelewa kuhusu rushwa ya ngono na namna ya kupambana nayo.
Aidha, amewataka wananchi wote wanaokumbana na vitendo vya rushwa, ikiwemo rushwa ya ngono, kutokubali kushawishiwa na badala yake kutoa taarifa kwa mamlaka husika ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.