Joy FM
Joy FM
18 November 2026, 10:44

Chemba ya Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC) Mkoa wa Kigoma, ikishirikiana pamoja na Enabel, imeendesha Mafunzo ya Manunuzi ya Umma kwa siku nne.
Mafunzo yameanza leo tarehe 17 hadi 20 Novemba 2026 katika ukumbi wa Kasulu Motel, Mafunzo haya yamewakutanisha wanawake na vijana 50 kutoka wilaya mbalimbali za Kigoma ikiwemo Kigoma mjini, Kasulu, Kibondo, Buhigwe na uvinza pamoja na wadau mbalimbali kutoka PPRA, TRA na Tender Bank.

Mafunzo haya yamelenga kuwajengea uwezo wanawake wafanyabiashara ili waweze kutambua fursa za zabuni, kuandaa nyaraka za maombi ya zabuni na kushiriki katika zabuni za Serikali na sekta binafsi.
Akizungumza katika ufunguzi, Bi. Rebecca Mpango, mwakilishi kutoka Ofisi ya Mkurugenzi halmashauri ya Kasulu Mji, aliipongeza TWCC kwa kuandaa mafunzo haya kwa kuwawezesha wanawake na vijana kiuchumi kwa kuwapatia maarifa, ujuzi na kuwaunganisha na fursa za kibiashara zinazoweza kusaidia kukuza biashara zao na kuongeza kipato.
Aidha, alihimiza washiriki kuwa pesa zipo NeST, hivo watumie nafasi hii vizuri kwa kushiriki kikamilifu, kuuliza maswali na kujifunza kwa vitendo.
Muhimu zaidi, wasiyachukulie mafunzo haya kama fursa ya kupata elimu tu, bali kama mwanzo wa kutumia maarifa watakayoyapata kukuza biashara zao na kufikia masoko mapya.
Ninatarajia kuwa baada ya mafunzo haya, tutashuhudia wanawake na vijana wengi zaidi wakishiriki katika zabuni na kupata mikataba ya kusambaza bidhaa na kutoa huduma kwa taasisi za umma na binafsi.