Joy FM

Shirika la posta latoa msaada taulo za kike kwa wafungwa gereza la Bangwe

8 October 2026, 13:23

Viongozi wa Posta wakikabidhi msaada kwa gereza la bangwe, Picha na Lucas Hoha

Uongozi wa gereza la bangwe lililopo Manispaa ya Kigoma Ujiji umesema umeendelea kushirikiana kwa pamoja na wadau na jamii katika shughuli zao

Na Lucas Hoha

Kuelekea maadhimisho ya siku ya Posta Duniani yanayofanyika kila Mwaka ifikapo tarehe 9 Oktoba Shirika la Posta Kigoma limetoa msaada wa vitu mbalimbali ikiwemo Sukari na taulo za Kike kwa wafungwa wa Gereza la Bangwe Manispaa ya Kigoma Ujiji Mkoani Kigoma ikiwa ni sehemu ya Shirika hilo kurudisha fadhila kwa jamii ili wafangwa wajionee ni sehemu ya jamii
Taarifa na Lucas Hoha

Akizungumza na waandishi wa habari Meneja wa Shirika la Posta Kigoma Ndagije Chobariko Pamoja na mambo mengine amesema Shirika la Posta ni miongoni mwa Mashirika hapa nchini ambayo yamekuwa yakiwajali wahitaji wa aina tofauti tofauti Wakiwemo Wajane na Watoto yatima.

Viongozi wa posta wakiwa kwenye picha na uongozi wa gereza la bangwe, Picha na Lucas Hoha

Wakati huohuo Ndagije ameongeza awamu hii wameona watoe msaada katika Gereza hilo kwani Shirika la Posta linatambua uwepo wa Wafungwa hao na changamoto mbalimbali zinazowakabili.

Kwa upande wake, Mrakibu Msaidizi wa Magereza Marry Leonsi mwendasila akimwakilisha Mkuu wa Gereza la Bangwe amesema Gereza hilo linapofanya majukumu ya kurekebisha tabia kwa wafungwa kwa kiwango kikubwa Wafungwa wanaamini kuwa Jamii inatambua uwepo wao, huku akitoa shukrani kwa Shirika la Posta kwa kutoa msaada huo.

Uongozi wa gereza la bangwe ukipokea msaada kutoka Shirika la posta, Picha na Lucas Hoha

Aidha ameongeza kuwa wafungwa hata kama ni wakosefu lakini pindi wanapoona misaada kutoka kwa wadau mbalimbali inawasaidia kubadili tabia zao wakiiamini kuwa jamii iko pamoja nao na inasaidia kubadili tabia zao nakuwa raia wema.