Joy FM

Wanavyuo watakiwa kujiepusha na vitendo vya ukatili Kasulu

12 November 2026, 13:09

Wanafunzi wa chuo cha ualimu Kasulu, Picha Hagai Ruyagila

Vitendo vya ukatili vimeendelea kujitokeza ambapo wito wa wadau pamoja na serikali wameendelea kutoa elimu ya namna ya kukomesha vitendo hivyo

Na Hagai Ruyagila

Wanafunzi wa Chuo cha Ualimu Kasulu kilichopo Halmashauri ya Mji Kasulu mkoani Kigoma, wametakiwa kujiepusha na vitendo vya ukatili wa kijinsia na badala yake kutoa taarifa kwa mamlaka husika wanapobaini vitendo hivyo ili kusaidia kukabiliana na tatizo hilo katika jamii.

Polisi Kata wa Kata ya Nyamnyusi, Willy Lupa, Picha na Hagai Ruyagila

Wito huo umetolewa na Polisi Kata wa Kata ya Nyamnyusi, Willy Lupa, wakati akizungumza na wanachuo hao katika utoaji wa elimu kuhusu ukatili wa kijinsia, maadili, uzalendo, amani na usalama wa taifa.

Amesema vitendo vya ukatili wa kijinsia vimeendelea kujitokeza katika jamii, hivyo amewahimiza wananchi kukemea vitendo hivyo na kutoa taarifa kwa viongozi wa serikali pamoja na viongozi wa dini ili kusaidia kupunguza na kuvitokomeza.

Kwa upande wake, Inspector, Nuru Maginga amewasisitiza wanachuo hao kutumia mitandao ya kijamii kwa kuzingatia sheria, kanuni na maadili ya Kitanzania, badala ya kuitumia kwa shughuli zinazoweza kuhatarisha amani na usalama wa jamii.

Inspector, Nuru Maginga, Picha na Hagai Ruyagila

Baadhi ya wanafunzi wa Chuo cha Ualimu Kasulu wamelishukuru Jeshi la Polisi kupitia kitengo cha Polisi Jamii Wilaya ya Kasulu kwa kutembelea chuoni hapo na kuwapatia elimu kuhusu masuala mbalimbali, ikiwemo ukatili wa kijinsia, maadili, uzalendo, amani na usalama.

Wamesema elimu waliyoipata itawasaidia kujenga uelewa na kuwa mabalozi wa kuelimisha wengine katika jamii kuhusu masuala hayo.

Mmoja wa wanachuo hao akichangia mada, Picha na Hagai Ruyagila