Joy FM
Joy FM
27 November 2026, 12:28

Wananchi Wilayani Kasulu kuhakikisha wanapanda miti ikiwa ni juhudi za kulinda mazingira
Na Hagai Ruyagila
Mkuu wa Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, Luteni Kanali Joseph Murimi, ameongoza zoezi la upandaji wa miti zaidi ya 200 katika Shule ya Msingi Mudyanda iliyopo Halmashauri ya Mji Kasulu, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kutunza mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Luteni Kanali Murimi amewahimiza wananchi kuwa na utamaduni wa kupanda miti katika maeneo yao, akieleza kuwa miti ina umuhimu mkubwa katika uhifadhi wa mazingira, kukuza uchumi na kupunguza hewa ukaa.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kasulu, Mwl. Vumilia Simbeye, amesema zoezi la upandaji miti limekuwa likitekelezwa katika halmashauri hiyo kwa kuhusisha taasisi mbalimbali na maeneo mengine, akibainisha kuwa upandaji wa miti ya matunda una mchango mkubwa katika kuongeza upatikanaji wa lishe bora kwa familia.

Afisa Mazingira wa Halmashauri ya Mji Kasulu, Wambura Mniko, ameeleza kuwa upandaji wa miti una faida nyingi, ikiwemo kuzuia mmomonyoko wa udongo, kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi, kuhifadhi mazingira na kuwawezesha wananchi kujipatia kipato.
Mwalimu wa Shule ya Msingi Mudyanda, Hidaya Omary, ameishukuru serikali kwa kuendesha zoezi hilo katika shule hiyo, akiahidi kuwa walimu na wanafunzi wataendelea kuitunza miti iliyopandwa ili iweze kukua na kuleta manufaa yaliyokusudiwa.

Baadhi ya wananchi walioshiriki katika zoezi hilo wamesema kuwa awali walikuwa na uelewa mdogo kuhusu uhifadhi wa mazingira, lakini kupitia elimu waliyoipata wameahidi kuitumia kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kupanda na kutunza miti.