Joy FM

Kigoma yaweka mikakati ya kukabiliana na el nino

24 November 2026, 16:14

Baadhi ya viongozi wa kamati hiyo wakiwa kwenye picha ya pamoja, Picha na Mwandishi wetu

Mvua zinazoendelea kunyesha Mkoani Kigoma zimesababisha athari mbalimbali ikiwemo nyumba na biashara mbalimbali kuharibika

Na Mwandishi wetu

Kamati ya Maafa ya Mkoa wa Kigoma, kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Idara ya Maafa, imeanza kuweka mikakati ya pamoja ya kuimarisha maandalizi na kukabiliana na athari zinzoweza kusababishwa na mvua za El Niño, ikiwemo uharibifu wa miundombinu na changamoto nyingine zinazoweza kuathiri maisha na shughuli za kiuchumi za wananchi.

Akifungua mafunzo hayo leo Novemba 24, 2026, katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko Mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, CPSP Patrick Kigere, amesema mafunzo hayo yanalenga kuweka mikakati ya pamoja itakayowezesha kukabiliana na majanga ya dharura na kupunguza athari zake kabla na wakati yanapotokea.

Baadhi ya viongozi wa kamati hiyo wakiwa kwenye picha ya pamoja, Picha na Mwandishi wetu

Aidha ameeleza mvua zinazoendelea kunyesha zinaweza kusababisha changamoto mbalimbali, ikiwemo uharibifu wa miundombinu na kuathiri shughuli za kijamii na kiuchumi, hivyo ameitaka Kamati ya Maafa kutumia mafunzo hayo kufanya tathmini na kuweka mikakati madhubuti ya kuzuia na kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.

Kwa upande wake, Mratibu wa Maafa Mkoa wa Kigoma, Bayanga Lukas,amesema kuwa mafunzo hayo yamewakutanisha wataalamu kutoka vitengo mbalimbali vya Serikali pamoja na wadau wa maendeleo ili kubadilishana uzoefu, kufanya tathmini na kuimarisha ushirikiano katika kuweka mazingira bora ya kushughulikia changamoto zinazoweza kuwakabili wananchi wakati wa majanga.

Baadhi ya viongozi wa kamati hiyo wakiwa kwenye picha ya pamoja, Picha na Mwandishi wetu

Naye mwezeshaji kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Maafa, Winfrida Ngowi, amesema maandalizi ya kukabiliana na maafa yanapaswa kufanyika mapema kwa kuwa majanga yanaweza kutokea wakati wowote na katika maeneo mbalimbali.

Amewashauri wajumbe wa Kamati ya Maafa kuendelea kutumia utaalamu wao kutoa ushauri na kuweka mikakati ya kukabiliana na majanga, hatua itakayosaidia kupunguza madhara kwa wananchi, mali zao na miundombinu.

Mafunzo hayo yanatarajiwa kuhitimishwa Novemba 27, 2026.