Joy FM

Shirika la posta laboresha utaoji wa huduma kwa wananchi Kigoma

12 October 2026, 15:44

Wadau mbalimbali wakiwa na viongozi wa posta wakikata keki ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya posta, Picha na Lucas Hoha

Wafanyabiashara na wananchi Mkoani Kigoma wameeleza kuwa huduma za posta zimerahisisha utumaji wa mizigo ndani na nje ya nchi

Na Lucas Hoha

Shirika  la posta Tanzania limesema litaendelea kushirikiana na zaidi ya nchi 200 duniani kwa lengo la kurahisisha huduma kwa wananchi wakati wa kutuma mizigo ili kuondoa usumbufu kwa wananchi wanapotuma mizigo hiyo kwenda nchi mbalimbali ikiwemo Marekani.

Meneja wa shirika la posta Mkoani Kigoma Bw. Ndagije Chobaliko amesema hayo wakati wa maadhimisho ya siku ya posta duniani  ambapo ameeleza kuwa shirika hilo litaendelea kuwahudumia wananchi kwa kuhakikisha huduma zinakuwa bora zaidi.

Aidha Chobaliko ametumia nafasi hiyo kuwashukuru wananchi kwa kuendelea kuliamini shirika hilo na kulitumia katika kutuma mizigo kwenda sehemu mbalimbali

Sauti ya Meneja wa posta Kigoma

Baadhi ya wakuu wa taasisi ambao wameshiriki maadhimisho hayo wamesema shirika la posta  limekuwa ni kimbilio la watu wengi pindi wanapotaka kusafirisha mizigo yao na masuala mengine ya kijamii,  huku wakiomba watumishi wa shirika hilo kuendelea kujituma ili kuwahudumia wananchi

Sauti ya wakuu wa taasisi

Hata hivyo baadhi ya wafanyabiashara na wadau ambao wamekuwa wakifanya kazi na shirika hilo pamoja na mambo mengine wamesisitiza umoja kati ya wananchi na shirika hilo uendelee kuwepo kwani shirika la posta Tanzania limeaminiwa na Serikali ili liweze kuwatumikia wananchi kwa kutuma migozo yao bila usumbufu.

Sauti ya wafanyabisahara

Maadhimisho ya siku ya posta duniani kwa mwaka huu yamebebwa na kauli mbiu isemayo ‘mtandao mmoja wa posta fursa zisizo na mwisho’.