Joy FM

Compassion kuwaunganisha wanafunzi vyuo mbalimbali nchini

17 November 2026, 14:51

Baadhi ya vijana ambao watanufaika na mpango huo, Picha na Lucas Hoha

Wanafunzi wameeleza kuridhishwa na mchango wa Compassion International Tanzania, wakisema shirika hilo limekuwa nguzo muhimu katika kuwaunganisha na fursa mbalimbali.

Na Lucas Hoha

Shirika la Compassion International Tanzania limeanzisha mpango maalumu wa kuwaunganisha wanafunzi wanaohitimu elimu ya sekondari, hususan Kidato cha Nne, na vyuo mbalimbali ili kuwawezesha kuendelea na masomo na kujikinga na vitendo viovu katika jamii, ikiwemo matumizi ya dawa za kulevya na mimba za utotoni zinazochangia kukatisha masomo kwa wanafunzi wa kike.

Mpango huo unalenga kuwapatia vijana fursa za elimu na kuwaweka katika mazingira salama yatakayowawezesha kutimiza ndoto zao badala ya kujiingiza katika changamoto zinazoweza kuathiri maisha yao ya baadaye.

Akizungumza wakati wa kongamano lililoandaliwa na shirika hilo, Emmanuel Musota kutoka Compassion International Tanzania, anayehudumia Cluster ya Kigoma Kaskazini na Wilaya ya Kasulu, amesema mpango huo tayari unawanufaisha zaidi ya wanafunzi 200 walio chini ya shirika hilo.

Musota amesema kuwa kuwaunganisha vijana na fursa za kujiendeleza kielimu ni hatua muhimu katika kuwajengea uwezo, kuwakinga na hatari mbalimbali za kijamii na kuwasaidia kufikia malengo yao.

Baadhi ya viongozi wakiwa katika kongamano hilo, Picha na Lucas Hoha

“Tunataka kuhakikisha vijana wanapata fursa za kuendelea na masomo yao na kuwa na mazingira bora yatakayowasaidia kujenga maisha yao ya baadaye badala ya kujiingiza katika vitendo vinavyoweza kuharibu ndoto zao,” amesema Musota.

Kwa upande wao, baadhi ya wadau walioshiriki kongamano hilo wamesema vijana wa sasa wana bahati ya kuwa na fursa nyingi za elimu na maendeleo ambazo hazikuwepo kwa kiwango hicho katika vizazi vilivyopita.

Wamewataka wanafunzi kutumia vizuri fursa hizo kwa kuzingatia masomo, kujituma na kuepuka vishawishi vinavyoweza kuwafanya washindwe kutimiza malengo yao.

“Vijana wa sasa wana fursa nyingi ambazo sisi hatukuwa nazo zamani na ni muhimu wazitumie vizuri kwa kuzingatia elimu na kujenga msingi imara wa maisha yao ya baadaye,” wameeleza baadhi ya wadau.

Nao wanafunzi walioshiriki kongamano hilo wameeleza kuridhishwa na mchango wa Compassion International Tanzania, wakisema shirika hilo limekuwa nguzo muhimu katika kuwaunganisha na fursa mbalimbali za elimu na maendeleo.

Wamesema baadhi yao wamekuwa wakipitia mazingira magumu ya maisha, lakini kupitia msaada wa shirika hilo wameweza kuendelea na masomo hadi kuhitimu, jambo ambalo hapo awali lilionekana kuwa gumu kutokana na changamoto walizokuwa wakikabiliana nazo.

“Compassion imekuwa msaada mkubwa kwetu kwa kutuunganisha na fursa mbalimbali. Baadhi yetu tumefanikiwa kumaliza masomo kupitia msaada wa shirika hili, licha ya changamoto za mazingira tuliyokuwa tunaishi,” wamesema wanafunzi hao.

Kongamano hilo limekuwa sehemu ya kuwakutanisha wanafunzi na wadau mbalimbali kwa lengo la kuwajengea uelewa kuhusu fursa za elimu, kuwaandaa kwa hatua zinazofuata baada ya kumaliza Kidato cha Nne na kuwahamasisha kufanya maamuzi sahihi yatakayolinda mustakabali wao.