Joy FM
Joy FM
6 October 2026, 14:02

Wakati wanafunzi wa kidato cha nne wakijianda kuanza mitihani yao, wazazi na walezi wametakiwa kuwa mstari wa mbele kuwasaidia watoto wao kutimiza ndoto zao
Na Emmanuel Kamangu
Wahitimu 100 wa Shule ya Sekondari Mikamba, iliyopo Kata ya Kidahwe katika Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma, wameahidi kufanya vizuri katika mitihani yao ya Kidato cha Nne, licha ya mitihani hiyo kusogezwa mbele kutokana na tishio la mvua za El Niño.
Wahitimu hao walitoa ahadi hiyo wakati wa mahafali yao ya nane yaliyofanyika shuleni hapo, ambapo pamoja na kusherehekea hatua hiyo muhimu ya maisha yao, waliwashukuru wazazi na walimu kwa ushirikiano waliowapa katika kipindi chao chote cha masomo.
Walisema mchango wa wazazi na walimu umekuwa muhimu katika kuwasaidia kufikia hatua hiyo na kuendelea kutimiza ndoto zao za kielimu.
Akizungumza katika mahafali hayo, mgeni rasmi, Meneja wa Exim Bank, Bw. Amatus Chuchumba, aliwasihi wahitimu hao kutumia fursa zinazotokana na utandawazi kwa ajili ya kujiendeleza kielimu na kimaisha, badala ya kuutumia katika mambo yasiyofaa.
Kwa upande wake, Meneja wa Shule ya Sekondari Mikamba, Bw. Ezra Mikamba, alisema licha ya mitihani ya Kidato cha Nne kusogezwa mbele kutokana na tishio la mvua za El Niño, ana imani wanafunzi hao watafanya vizuri kwa kuwa wameandaliwa ipasavyo.
Naye Mkuu wa Shule hiyo, Bw. James Kivula, aliwataka wahitimu kuendelea kusoma kwa bidii na kuzingatia nidhamu ili kuendeleza sifa njema ya shule hiyo katika kupata matokeo mazuri, kama ilivyokuwa kwa wahitimu waliowatangulia.
Mahafali hayo ni ya nane tangu kuanzishwa kwa Shule ya Sekondari Mikamba mwaka 2016. Shule hiyo imeendelea kukua na kupanua huduma zake za elimu, huku uongozi ukipanga kuanzisha shule ya msingi katika eneo hilo kwa lengo la kuongeza wigo wa upatikanaji wa elimu kwa jamii inayozunguka.