Joy FM

Watumishi wa umma waaswa kupima afya ya akili Kigoma

20 November 2026, 09:48

Baadhi ya watumishi wakiwa kwenye mafunzo hayo, Picha na Mwandishi wetu

Matatizo ya afya ya akili ni changamoto kubwa katika jamii kwa sababu yanaathiri maisha ya mtu binafsi, familia na taifa kwa ujumla

Mwandishi wetu

Watumishi wa Umma Mkoani Kigoma wametakiwa kujiwekea utaratibu wa kupima Afya ya Akili angalau mara mbili kwa mwaka, hali itakayowasaidia kufanya maamuzi sahihi kwenye maisha yao pamoja na kutoa huduma bora kwa wananchi.

Wito huo umetolewa na Msaikolojia kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Maweni-Kigoma Dkt. Elen Ndekenga, alipotoa mafunzo kwa watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kigoma, kuhusu umuhimu wa kudumisha usalama wa afya ya akili mahala pa kazi.

Amesema, inapotokea Mtumishi anashindwa kutekeleza majukumu yake ya kila siku kwa ufanisi akiwa ndani au nje ya Ofisi, hali hiyo huashiria  uwepo wa dalili ya changamoto ya afya ya akili kwa mtendaji huyo.

Msaikolojia kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Maweni-Kigoma Dkt. Elen Ndekenga, Picha na Mwandishi wetu

Amesema dalili za changamoto ya Afya ya akili hujitokeza kupitia fikra, hisia, mwenendo wa mwili na tabia binafsi za mtu, zinazoweza kusababisha kuhisi kuugua, kuibuka kwa hisia tofauti tofauti pamoja na kujijengea  tabia za kipekee.

Amevitaja visababishi vya changamoto ya afya ya akili kuwa ni pamoja na muhusika kukabiliana na matukio ya kushtua hisia, hitilafu katika mfumo wa ubongo, matumizi ya kupitiliza ya pombe au dawa za kulevya.

Ameendelea kutaja visababishi vingine kuwa ni matumizi ya kupitiliza ya mitandao ya kijamii, kutazama picha za ngono pamoja na kujikita katika michezo ya Kamali.

Baadhi ya watumishi wakiwa kwenye mafunzo hayo, Picha na Mwandishi wetu

Amesema sambamba na kupatiwa ushauri wa kitaalam, wanaobainika na shida hiyo, wanapaswa kubadili mitindo yao ya maisha na kuepuka visababishi.

Awali akifungua mafunzo hayo, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Dkt. Damas Kayera amesema suala la watumishi wa Umma kutambua hali zao za afya ya akili ni muhimu kwani wanajukumu kubwa katika kuhudumia jamii.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Dkt. Damas Kayera, Picha na Mwandishi wetu

“Utimamu wa akili kwa watendaji wetu ni suala la msingi sana kwani wao ndio wenye jukumu la kusimamia na kutekeleza majukumu mbalimbali yaliyowekwa na serikali kwa ajili ya kutoa huduma na kusukuma gurudumu la Maendeleo ya taifa” amesema Kayera.

Pamoja na mafunzo hayo, Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, imeendesha zoezi la upimaji wa afya kwa watumishi wa ofisi ya Mkuu wa mkoa, kwa lengo la kuwawezesha kujua hali zao na kuchukua hatua ili kujilinda dhidi ya maradhi mbalimbali.

Baadhi ya watumishi wakiwa kwenye mafunzo hayo, Picha na Mwandishi wetu