Joy FM

Wanaume Kigoma wavunja ukimya kuripoti ukatili wa kijinsia

17 November 2026, 16:22

Muonekan wa baadhi ya wanaume wanaojitokeza kuripoti vitendo vya ukatili, Picha na Joy Fm

Wanaume Mkoani Kigoma wameanza kujitokeza zaidi kuripoti vitendo vya ukatili wa kijinsia wanavyofanyiwa, hali inayotajwa kuchangiwa na ongezeko la elimu kuhusu haki za binadamu na umuhimu wa kupinga ukatili katika jamii.

Kwa muda mrefu, vitendo vya ukatili wa kijinsia vimekuwa vikihusishwa zaidi na wanawake na watoto, huku wanaume wengi wakibaki kimya wanapokumbana na vitendo hivyo kutokana na hofu, aibu na mitazamo hasi ya kijamii.

Hata hivyo, hali hiyo inaonekana kubadilika mkoani Kigoma, ambako mwitikio wa wanaume kujitokeza kuripoti matukio ya ukatili wa kijinsia umetajwa kuongezeka siku hadi siku.

Selemani Yusuph (si jina lake halisi), baba wa watoto wanne na mkazi wa Kata ya Rusimbi, Manispaa ya Kigoma Ujiji, ni miongoni mwa wanaume waliowahi kukumbana na vitendo vya ukatili wa kijinsia na kuamua kuvunja ukimya kwa kutafuta haki.

Baadhi ya wanaume waliozungumza na Radio Joy FM wamesema mwitikio wa wanaume kuripoti ukatili umeongezeka ikilinganishwa na miaka ya nyuma. Wameeleza kuwa elimu inayotolewa kuhusu ukatili wa kijinsia imewasaidia kutambua vitendo hivyo na kuwajengea ujasiri wa kujitokeza kutoa taarifa.

Wamesisitiza kuwa kuripoti vitendo vya ukatili si udhaifu, bali ni hatua muhimu ya kudai haki, kupata msaada na kuchangia kukomesha vitendo hivyo katika jamii.

Akizungumzia hali hiyo, Michael Mjema, Mrakibu Msaidizi wa Jeshi la Polisi na Mkuu wa Dawati la Jinsia na Ulinzi wa Mtoto Mkoa wa Kigoma, amesema dawati hilo limeanzishwa kwa lengo la kutoa huduma kwa watu wote bila ubaguzi wa kijinsia.

Amesema huduma zinazotolewa zinawalenga wahanga wote wa ukatili, wakiwemo wanaume, wanawake na watoto, huku akisisitiza umuhimu wa wananchi kujitokeza kutoa taarifa wanapokumbana na vitendo hivyo.

Kwa ujumla, kuongezeka kwa mwitikio wa wanaume kuripoti ukatili wa kijinsia mkoani Kigoma ni hatua muhimu katika mapambano dhidi ya vitendo hivyo.

Jamii inahimizwa kuachana na mitazamo inayowafanya wanaume waogope kuzungumza wanapokuwa wahanga wa ukatili, na badala yake kuwapa nafasi ya kupata msaada, ulinzi na haki bila kujali jinsia zao.