Joy FM
Joy FM
10 November 2026, 10:10

Serikali imesema itaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo katika kuboresha huduma za afya nchini
Na Mwandishi wetu
Mradi wa mjamzito na mtoto salama unaotekelezwa na shirika la Thamini uhai umetajwa kuleta matokeo chanya kwa kupunguza vifo vya mama na mtoto wakati wa kujifungua katika hospitali ya Mji Kasulu na kituo cha afya kiganamo mkoani Kigoma.
Akizungumza baada ya kufanyika kwa ziara ya Kamati ya Bunge ya afya na masuala ya Ukimwi Naibu waziri wa Afya Dkt Frolence Samizi amesema Serikali inalenga kupunguza vifo vya mama na mtoto kufikia mwaka 2030.

Amesema mradi wa usindikizaji wa mama mjamzito umesaidia kujenga uaminifu na upendo ambapo mama mjamzito huchagua mtu anayehitaji kuwa naye karibu wakati wa kujifungua akisisitiza kuwa serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya afya.
Mwenyekiti wa kamati ya Bunge afya na masuala ya Ukimwi Dkt.Emmanuel Qambaji Nuwas ameupongeza mkoa wa Kigoma kwa kufanikiwa kupunguza vifo vya mama na mtoto huku akisisitiza umuhimu wa wahudumu wa afya kuzingatia maadili ya kazi na kutumia lugha nzuri kwa wagonjwa.
Mkurugenzi wa Shirika la Thamini uhai Banzi Msumi ameeleza kuwa shirika hilo litaendelea kusimamia masuala ya afya kwa kutoa maelekezo kwa vituo vya afya na hospiatli ikiwa ni pamoja na kuongeza uwekezaji katika vituo vya kutolea huduma za afya ili kufikia malengo ya kupunguza vifo vya mama na mtoto.