Storm FM
Storm FM
10 November 2026, 6:09 pm

Halmashauri hiyo imefanikiwa kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 11.9 katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2026/2027
Na Mrisho Sadick:
Halmashauri ya Manispaa ya Geita mkoani Geita inatekeleza miradi 17 ya kimkakati kwa kutumia fedha za mapato ya ndani kati ya miradi 29 inayotekelezwa kwa vyanzo mbalimbali vya fedha ikiwemo fedha kutoka Serikali Kuu na vyanzo vingine.
Mkuu wa Wilaya ya Geita Hashim Komba akiwa katika kikao cha robo ya kwanza cha baraza la madiwani wa Manispaa ya Geita leo Novemba 10,2026 ameipongeza Manispaa hiyo kwa hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa miradi hiyo akieleza kuwa mafanikio hayo yanachangiwa na kasi ya ukusanyaji wa mapato pamoja na ubunifu wa vyanzo vipya vya mapato ambavyo havileti kero kwa wananchi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Geita Yefred Myenzi amesema halmashauri hiyo imefanikiwa kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 11.9 katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2026/2027 hatua inayotarajiwa kusaidia miradi inayofadhiliwa kwa mapato ya ndani kukamilika kwa wakati.
Naye Mwenyekiti wa Manispaa ya Geita Leonard Kiganga Bugomola pamoja na Mbunge wa Jimbo la Geita Mjini Chacha Wambura wameeleza kuridhishwa na kasi ya utekelezaji wa miradi ya kimkakati huku wakiwapongeza wataalamu wa halmashauri kwa juhudi zao katika kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo.

Miongoni mwa miradi hiyo ni ujenzi wa jengo la kitega uchumi la Gedeco Tower , ujenzi wa miundombinu ya barabara pamoja na ujenzi wa Uwanja wa Mpira wa Magogo na miradi mingine ya maendeleo inayolenga kuongeza fursa za kiuchumi na kuboresha huduma kwa wananchi.