Storm FM

Kemikali ya zebaki tishio kwa wachimbaji Geita

3 May 2024, 7:43 pm

Moja ya sehemu ya shughuli za usagaji na uchenjuaji wa madini ya dhahabu katika kata ya Mgusu wilayani Geita. Picha na Mrisho Sadick

Kukosekana kwa mbadala wa kemikali yenye gharama nafuu ya uchenjuaji wa madini ya dhahabu, imeendelea kuziweka rehani afya za wachimbaji wa madini mkoani Geita kwa kutumia kemikali ya zebaki yenye madhara kiafya.

Na Mrsiho Sadick – Geita:

Serikali imeanza kutoa mafunzo kwa wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu mkoani Geita juu ya matumizi sahihi ya kemikali ya zebaki wanayoitumia kukamatia madini hayo kwa kuwa ina madhara  kiafya ikiwemo kusababisha upofu.

Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali imepewa jukumu la kutoa elimu ya matumizi salama ya kemikali ya zebaki kutokana na utekelezaji wa sheria namba tatu ya 2003 inayohusu usimamizi na udhibit wa kemikali za viwandani na majumbani ikiwemo zebaki.

Meneja wa usajili wa kemikali na maabara za kemia kutoka ofisi ya mamlaka ya maabara ya mkemia mkuu wa serikali Musa Kuzumila. Picha na Mrisho Sadick

Akiwa katika mafunzo ya matumizi sahihi ya kemikali hiyo kwa wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu katika Kata ya Mgusu wilayani Geita meneja wa usajili wa Kemikali na Maabara za Kemia kutoka ofisi ya mamlaka ya maabara ya mkemia mkuu wa Serikali Musa Kuzumila  amesema serikali imeamua kuanzisha mafunzo hayo ili kuwaepusha wachimbaji na madhara ya kiafya.

Sauti ya meneja usajili wa kemikali
Wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu wakiwa katika mafunzo ya matumizi ya Zebaki katika kata ya Mgusu wilayani Geita. Picha na Mrisho Sadick

Kwa upande wake Mkemia kutoka mamlaka ya maabara ya mkemia mkuu wa serikali Derick Masako amesema miongoni mwa madhara ya kiafya ambayo mchimbaji anaweza kuyapata kwa kutumia kemikali ya zebaki bila kufuata utaratibu ni pamoja na kupata upofu.

Sauti ya mkemia mamlaka ya maabara nchini

Akizungumza kwa niaba ya wachimbaji katika mafunzo hayo Dafroza Lugendo amesema wanaipongeza serikali kwa kuandaa mafunzo hayo kwani hapo walikuwa wanatumia kemikali hiyo holela huku afisa mazingira kutoka ofisi ya Mkoa wa Kimadini Geita  Yasinta Laurian akisema mpango huo unalengo la kuwakomboa wachimbaji.

Sauti ya wachimbaji na afisa mazingira

Baraza la taifa la hifadhi na usimamizi wa mazingira NEMC unatekeleza  mkataba wa MINAMATA kuandaa mpango kazi na kuhakikisha inadhibiti matumizi ya zebaki nchini.