Storm FM

Mkuu wa mkoa Geita akagua miradi ya mwenge Mbogwe

20 July 2023, 11:05 am

Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa wa Geita ikiwa wilayani Mbogwe. Picha na Mrisho Sadick

Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita yajipanga kuupokea mwenge wa uhuru kwa kuanza ukaguzi katika miradi yote itakayopitiwa.

Na Mrisho Sadick:

Mkuu wa mkoa wa Geita, Martin Shigela ameiongoza Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa, Kamati ya Ulinzi na Usalama wilaya ya Mbogwe, wakuu wa Idara na Vitengo Halmashauri hiyo na kukagua miradi ya maendeleo inayotarajiwa kuzinduliwa na kuwekwa mawe ya msingi na Mwenge wa Uhuru mwaka huu.

Shigela ameipongeza wilaya ya Mbogwe kwa miradi mizuri na kushauri maandalizi yanayoendelea yakamilike kwa wakati pamoja na hamasa kwa wananchi katika maeneo yote yatakayopitiwa na mwenge kuanzia eneo la mapokezi mpaka eneo la mkesha ifanyike.

Wilaya ya Mbogwe inatarajia kupokea mbio za mwenge wa uhuru Agosti 5, 2023 katika viwanja vya shule ya msingi Lulembela.

Mradi wa ujenzi wa zahanati utakaopitiwa na Mwenge wa Uhuru Mbogwe. Picha na Mrisho Sadick

Naye mkuu wa wilaya ya Mbogwe, Sakina Mohamed na Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri hiyo, Saada Mwaruka wamemshukru Mkuu wa Mkoa Shigela kwa ziara hiyo na kuahidi utekelezaji katika maagizo yote aliyoyatoa.