Storm FM

Mradi wa Kata 5 kunufaisha watu zaidi ya laki moja Geita

20 January 2024, 9:48 am

Kamati ya siasa ya Halmashauri kuu ya CCM Geita ikiwa katika ukaguzi wa mradi wa Kata 5. Picha na Bashiru Said

Serikali imedhamiria kumaliza changamoto ya maji kwa kuendelea kutekeleza miradi mikubwa ya maji hususani vijijini.

Mrisho Shabani:

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan ametoa Bilioni 10.8 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa maji wa Kata tano zilizokuwa zikikabiliwa na Changamoto hiyo licha ya kuwa karibu na ziwa Victoria wilayani Geita.

Akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi huo mbele ya Kamati ya siasa ya Halmashauri Kuu ya CCM wilaya ya Geita Kaimu meneja wa RUWASA wilaya ya Geita Pius Didackus amesema kukamilika kwa mradi huo kutawanufaisha watu laki moja na Elfu 24 na 629 huku awamu ya kwanza ukianza na Kata za Katona na Nkome huku diwani wa kata ya Katoma Josephat Komanya akiomba wananchi wa eneo hilo washirikishwe kwa kupewa ajira za muda kwenye utekelezaji wa mradi huo.

Kamati ya siasa ya Halmashauri kuu ya CCM Geita ikiwa katika ukaguzi wa mradi wa Kata 5. Picha na Bashiru Said

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Geita Cornel Magembe akiwa kwenye ziara hiyo amesema zoezi la utandazaji wa mabomba umeanza na umefikia urefu wa kilometa zaidi moja.

Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Geita Barnabas Mapande ameipongeza serikali kwa dhamira yake ya kumtua ndoo Mama huku akiagiza mradi huo ukamilike mwezi wa sita kwa mujibu wa mkataba wa Utekelezaji.

Mradi huo unatekelezwa kwenye Kata za Nkome , Katoma , Nyamboge, Rwezera na Nzera wilayani Geita.