Storm FM

Geita yakabidhi Mwenge wa Uhuru Kagera

8 August 2023, 7:37 pm

Mkuu wa Mkoa wa Geita kushoto akimkabidhi Mwenge wa Uhuru Mkuu wa Mkoa wa Kagela aliye kulia Fatuma Mwasa. Picha na Mrisho Sadick

Mbio za Mwenge wa Uhuru zimefikia tamati Mkoani Geita baada ya kukimbizwa kwa siku sita katika Halmashauri sita za Mkoa huo kuanzia agosti 2 hadi 8 mwaka huu.

Na Mrisho Sadick:

Mkuu wa Mkoa wa Geita Martine Shigela amemkabidhi Mwenge wa Uhuru Mkuu wa Mkoa wa Kagera Fatuma Mwasa kwa ajili ya kuukimbiza katika Mkoa huo kuanzia leo agosti 08-2023.

Mwenge wa Uhuru ulipokuwa Mkoani Geita umekimbizwa Kilometa 755 katika Halmashauri sita za Nyang’hwale,Geita Mji,Geita DC, Mbogwe,Bukombe na Chato nakupitia miradi 59 yenye thamani ya Shilingi bilioni 29, kati ya miradi hiyo mmoja wa Zahanati ya Shinamwenda Halmashauri ya Mji wa Geita haukuzinduliwa kutokana na dosari nyingi zilizobainika.

Wilaya ya Chato ndio Halmashauri ya mwisho kuukimbiza Mwenge wa Uhuru ambapo ulipitia miradi saba yenye thamani ya Shilingi bilioni 13 ukiwemo mradi wa shamba la Miti la Silayo uliyotumia zaidi ya Bilioni 11 kupanda nakuhifadhi miti milioni 5 iliyopandwa kuanzia Mwaka 2017.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Abdalla Shaib ameridhishwa na Utekelezaji wa mradi huo huku Afisa Mazingira Kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais Joseph Kiwango akisisitiza suala la utunzaji wa mazingira.

Zoezi la makabidhiano limefanyika katika viwanja vya shule ya Sekondari Nyakabango wilayani Muleba, Mwenge wa Uhuru ukiwa Mkoani Kagera utakimbizwa umbali wa Kilometa 1,200.4 na utapitia miradi 57 yenye thamani ya Shilingi bilioni 26.3.