Storm FM

Wachimbaji na wavuvi hawatumii vyoo kisa imani potofu

28 January 2024, 12:55 pm

Wajumbe wa idara ya afya wakiwa kwenye kikao cha tathimini ya afya Mkoani Geita . Picha na Edga Rwenduru

Makundi ya wachimbaji na wavuvi yako hatarini kupata magonjwa ya mlipuko hususani kipindupindu kwasababu hawatumii vyoo kwenye maeneo yao.

Na Mrisho Shabani:

Wachimbaji wa madini ya dhahabu pamoja na wavuvi mkoani Geita wametajwa kuwa ni miongoni mwa makundi ambayo hayana utamaduni wa kutumia vyoo kutokana na imani potofu kuwa wakitumia vyoo uzalishaji wao unapungua.

Hayo yamebainishwa na Katibu tawala wa mkoa wa Geita Mohammed Gombati wakati wa ufunguzi wa kikao cha idara ya afya mkoani Geita kutathimini mafanikio na changamoto zinazoikumba idara hiyo huku akiagiza idara ya afya kuwekeza nguvu ya kutoa elimu kwa makundi hayo mawili.

Sauti ya Katibu tawala Mkoa wa Geita
Katibu tawala wa mkoa wa Geita akizungumza kwenye kikao cha idara ya afya . Picha na Edga Rwenduru

Aidha kwa upande wake Mganga mkuu wa mkoa wa Geita Dokta Omary Sukari ameagiza maeneo yote ya myalo pamoja na migodi lazima kuwepo na vyoo bora.

Sauti ya Mganga Mkuu wa Mkoa

Uongozi wa Chama cha wachimbaji wadogo mkoani Geita GEREMA wameanza ziara ya kutembelea migodi ili kutoa elimu ya kuzingatia usafi maeneo ya migodini.