Storm FM

EWURA CCC Geita yazitahadharisha taasisi, kampuni kuzingatia haki ya mteja

1 October 2023, 7:09 pm

Ofisa Tawala Msaidizi kutoka EWURA CCC mkoa wa Geita, Wadi Omari. Picha na Zubeda Handrish

Kupitia maonesho ya 6 ya kimataifa ya madini EWURA CCC iliendelea kutoa huduma ya kupokea malalamiko na kuyafanyia kazi kutoka kwa wateja wa huduma ya nishati na maji, wingi wa malalamiko yalipelekea EWURA CCC kutoa tahadhari.

Na Zubeda Handrish- Geita

Ofisa Tawala Msaidizi kutoka EWURA CCC Wadi Omari, kupitia Baraza la Ushauri na Utetezi wa Watumiaji wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA CCC) amezitaka mamlaka na taasisi za huduma hizo kuzingatia kanuni, taratibu na haki ya wateja wanapotoa huduma.

ameyasema hayo jana Septemba 30 alipozungumza na waandishi wa habari katika viwanja vya maonyesho ya sita ya kimataifa ya teknolojia ya madini EPZA, Bombambili mjini Geita yaliyokamilikan jana.

Ofisa huyo amesema mbali na kutoa huduma ana wajibu wa kutambua mteja wake ana haki ya kupewa huduma sahihi, stahiki na kwa wakati pindi anapolipia na inapotokea dharura afahamishwe.

Ametolea mfano mtu anapolipia huduma ya umeme anapaswa ndani ya siku 30 za kazi awe ameunganishiwa, na endapo kuna changamoto basi mteja aarifiwe vinginevyo ni ukiukaji wa haki.

Amesema , kanuni ya utoaji huduma inaelekeza iwapo mtoa huduma atachewesha kuunganisha huduma ya maji na umeme atapaswa kumfidia mteja wake kwa pesa taslimu ama kihuduma.

Ameahidi EWURA CCC inaendelea kuwasiliana na mamlaka husika ili kutatua malalamiko huku akiwataka watanzania kufuata taratibu za utoajia malalamiko badala ya kubaki na manung’uniko nyumbani.