Storm FM

Vijana washauriwa kutobagua kazi za kufanya Geita

23 April 2021, 6:15 pm

Na Ester Mabula:

Vijana mkoani Geita wameshauriwa kujiajiri na kuacha dhana ya kubagua kazi ili kuweza kujipatia maendeleo  na kuendesha maisha yao.

Hayo yamebainishwa na baadhi ya vijana walioamua kujiajiri kwa kuunda kikundi cha  kutengeneza bidhaa mbalimbali kwa kutumia vyuma chakavu ikiwemo majiko sanifu katika mtaa wa Nyankumbu uliopo katika Halmashauri ya mji wa Geita na kuongeza kuwa miongoni mwa sababu zinazopelekea vijana wengi kushindwa kufikia mafanikio ni kubagua kazi  pamoja na kuishi maisha ya kuiga.

Vijana waliojiajiri

Mbali na kuwahimiza vijana kuendelea kuchapa kazi na kuachana na dhana ya kutegemea kuajiriwa, vijana hao wametoa rai kwa vijana wenzao kutumia ujuzi walionao kwakuwa ujuzi ni mtaji na fursa za uzalishaji mali zinapatikana kwa kujituma, kuwajibika na kutanguliza uaminifu au adilifu katika kazi .