Storm FM

Kufariki kwa mjamzito Busanda wananchi waiangukia serikali

16 April 2024, 3:49 pm

Mwonekano wa zahanati ya Lubando ambayo wananchi wanaomba ianze kutoa huduma. Picha na Edga Rwenduru

Uhaba wa vituo vya afya kwa baadhi ya maeneo ya mkoa wa Geita umeendelea kusababisha changamoto mbalimbali ikiwemo vifo vya akina mama wajawazito na watoto.

Na Edga Rwenduru – Geita

Wakazi wa kijiji cha Lubanda kata ya Busanda wilayani na mkoani Geita wameiomba serikali kuwasaidia zahanati iliyojengwa kwa nguvu za wananchi katika eneo hilo ianze kufanya kazi kwani tayari imekamilika na haitoi huduma.

Baadhi ya wakazi hao Marietha Thomas , Mayala Magili na Tatu Masele wamesema hayo wakati wakizungumza na Storm FM kufuatia tukio la mama mjamzito kufariki dunia baada ya kujifungulia njiani wakati anaelekea kituo cha afya Katoro kilicho umbali wa zaidi ya kilometa 10 kutoka katika kijiji hicho.

Sauti ya wananchi wa Lubanda
Baadhi ya wakazi wa Lubanda wakiwa katika msiba wa mama mjamzito aliefariki baada ya kujifungulia njiani. Picha na Edga Rwenduru

Mwenyekiti wa kijiji hicho Charles Lile amesema kinachokwamisha zahanati hiyo kutoa huduma mpaka sasa ni kutokamilika kwa jengo la watumishi ambalo linajengwa kwa kutumia fedha za CSR.

Sauti ya mwenyekiti wa Lubanda

Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Geita Karia Rajabu amesema ofisi yake haijapata taarifa ya uwepo wa tukio hilo nakuwataka viongozi wa kijiji hicho kuwasilisha maombi ya kuanza kazi kwa zahanati hiyo ili kuepukana na changamoto kama hiyo.

Sauti ya mkurugenzi Geita DC

Mkuu wa wilaya ya Geita Hashim Komba hivi karibuni aliahidi kufanya kikao cha pamoja na wasimamizi wa miradi ya CSR ambayo imechelewa kukamilika kwa wakati licha ya fedha hizo kutolewa.

Sauti ya mkuu wa wilaya ya Geita