ACT wazalendo walalamikia bendera zao kushushwa
7 July 2023, 7:33 pm
Katibu wa ACT- Wazalendo amekuja juu na kutoa shutuma baada ya bendera kadhaa za chama chao kushushwa katika mitaa na barabara za mjini Geita, jambo lililopelekea Katibu wa chama hicho kuzungumzia hilo.
Na Said Sindo- Geita
Bendera za chama cha ACT- Wazalendo mkoa wa Geita zilizokuwa zimewekwa katika barabara na mitaa mbalimbali zimeshushwa na watu wasiojulikana usiku wa manane wa kuamkia Julai 5, 2023.
Akizungumza na waandishi wa habari katibu wa chama hicho mkoa wa Geita Emmanuel Ikolongo Otto, amesema kushushwa kwa bendera hizo kuna mkono wa mtu, kwa madai kuwa wingi wa bendera hizo unaonesha uhalali na uhai wa chama hicho kwenye maeneo hayo.
Uamuzi huo umeonekana kuwashtua viongozi wa chama hicho huku wakikitupia lawama Chama cha mapinduzi kuwa ndio kilichosuka mpango huo.
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Geita Berthaneema Mlay alipotafutwa kuzungumzia malalamiko hayo, amesema jeshi la polisi halijapokea taarifa yoyote ya kushushwa kwa bendera za chama hicho.
Ikumbukwe kuwa kushushwa kwa bendera hizo kumekuja siku chache tu baada ya kumalizika kwa mkutano mkuu wa Chama hicho uliofanyika nyankumbu ukiongozwa na kiongozi wa chama hicho Zitto Kabwe ambapo bendera hizo ziliwekwa katika barabara za maeneo tofauti kabla ya mkutano huo.