Storm FM

Akamatwa akituhumiwa kunajisi kanisa, lafungwa siku 30

7 September 2023, 10:21 pm

Kanisa la Mtakatifu Bernadetha wa Lurd Parokia ya Nyakato-Buzrayombo. Picha na Zubeda Handrish

Tukio la kunajisiwa Kanisa ni la pili kutokea mkoani Geita ikiwa ni miezi sita imepita baada ya kijana mmoja mkazi wa Geita kudaiwa kuvamia Kanisa Kuu la Kiaskofu Jimbo la Geita na kufanya uharibifu uliosababisha hasara ya Sh. milioni 48.2.

Na Zubeda Handrish- Geita

Mkazi wa Chato, John Marore anashikiliwa na Jeshi la Polisi wilayani humo kwa tuhuma za kuvamia makanisa mawili likiwemo la Mtakatifu Bernadetha wa Lurd Parokia ya Nyakato-Buzrayombo na lile la Waadventisti wasabato yaliyopo kata ya Buzrayombo mkoani Geita.

Matukio ya uhalifu kwenye makanisa hayo yalitokea usiku wa Septemba Mosi, 2023 na kusababisha Kanisa la Mtakatifu Bernadetha wa Lurd kufungwa kwa siku 30 kutokana na kufuru na najisi iliyofanywa ndani ya Kanisa hilo.

Mkuu wa Wilaya ya Chato, Deusdedith Katwale amethibitisha kukamatwa kwa mtu huyo akidai Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi kubaini wote waliohusika  ili sheria ichukue mkondo wake.

Sauti ya Mkuu wa Wilaya ya Chato, Deusdedith Katwale

Katika taarifa iliyotolewa Septemba Mosi na Makamu wa Askofu jimbo la Rulenge –Ngara Padri Ovan Mwenge ilieleza watu wasiojulikana walivunja ukuta wa kanisa na kufanya kufuru kwenye sakramenti ya Ekaristi Takatifu kwa kuila ama kuondoka nayo na nyingine kuitelekeza sakafuni ndani na nje ya kanisa.

Kanisa la Mtakatifu Bernadetha wa Lurd Parokia ya Nyakato-Buzrayombo. Picha na Zubeda Handrish

Kwa sasa waumini wanasali nje ya kanisa hilo wakihimizwa kusali, kufunga, kufanya toba na malipizi kwa Mwenyezi Mungu ili aboreshe mioyo ya watu wenye nia ovu kwa mambo matakatifu.

Wakazi na waumini wa Kanisa lililonajisiwa na kufungwa siku 30
Wakazi na waumini wa Kanisa lililonajisiwa na kufungwa siku 30

Taarifa hiyo ilieleza maelekezo na sheria ya Kanisa kanuni ya 1211 -1213 na kwa maelezo ya Askofu Severine Niwemugizi kanisa hilo litafungwa kwa siku 30 ambapo baada ya maboresho na ukarabati mdogo, litabarikiwa na kutakaswa ili liendelee kutumika.