Storm FM

Aliyechomewa Gari Geita ameipongeza Ripoti ya tume ya uchunguzi

23 April 2026, 10:45 pm

Neema Erasimo mkazi wa Geita na mhanga wa matukio ya Oktoba 29 akizungumzia Ripoti hiyo. Picha na Mrisho Sadick

Matumaini makubwa ya wananchi wa Geita kupitia Ripoti ya uchunguzi ni taifa kuimarisha mshikamano, amani, na imani ya wananchi kwa serikali yao.

Na Mrisho Sadick:

Baada ya Tume ya Uchunguzi wa Matukio ya Oktoba 29 kuwasilisha ripoti yake kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan, baadhi ya wananchi mkoani Geita wameipokea hatua hiyo kama mwanzo wa uponyaji wa taifa.

Miongoni mwa walioathiriwa na vurugu hizo ni Neema Erasimo mkazi wa Manispaa ya Geita ambaye gari lake lilichomwa moto ameeleza kuwa ripoti ya tume hiyo imempa matumaini mapya na kuiona kama hatua muhimu kuelekea haki na maridhiano.

Fred Fidel Mwenyekiti wa Maafisa Usafirishaji Mkoa wa Geita akizungumzia Ripoti ya tume ya uchunguzi wa matukio ya Oktoba 29. Picha na Mrisho Sadick

Kwa upande wake Fred Fidel Mwenyekiti wa Maafisa Usafirishaji Mkoa wa Geita pamoja na Hajat Mariam Sharif kiongozi wa dini wameeleza imani yao kuwa mapendekezo yaliyomo kwenye ripoti hiyo yatapewa uzito unaostahili huku wakisisitiza kuwa utekelezaji wake unaweza kuleta mabadiliko chanya katika mifumo ya uongozi, kuimarisha uwajibikaji, na kuongeza usalama wa raia.

Hajat Mariam Sharif Mkazi wa Mkoa wa Geita akizungumzia Ripoti ya tume ya uchunguzi wa matukio ya Oktoba 29. Picha na Mrisho Sadick

Kwa ujumla wananchi wa mkoa wa Geita wameipongeza kwa dhati hatua ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuunda tume hiyo, wakieleza kuwa imeonesha dhamira ya serikali katika kusikiliza kilio cha wananchi, kutafuta ukweli, na kuweka msingi wa haki na maridhiano.

Sauti ya Wananchi Mkoani Geita