Storm FM

Vijana 1,056 Geita wahitimu mafunzo ya polisi jamii yaliyofadhiliwa na GGML

19 June 2026, 8:04 pm

Kampuni ya GGML imekuwa mdhamini wa mafunzo ya polisi jamii mkoani Geita tangu mwaka 2016 ikiwa ni sehemu ya mchango wake katika kuimarisha usalama na maendeleo katika ya jamii zinazouzunguka mgodi.

Na: Ester Mabula

Vijana 1056 kutoka katika mitaa 7 inayozunguka Mgodi wa Geita Gold Minning Limited (GGML) wamehitimu mafunzo ya polisi jamii leo Juni 19, 2026 ili kuendelea kuimarisha ulinzi na usalama katika mitaa yao.

Mafunzo hayo yamefadhiliwa na Kampuni ya GGML kwa kushirikiana na Jeshi la polisi ambapo Mkurugenzi mtendaji wa mgodi wa GGML Ashraf Suryaningrat amesema mgodi huo utaendelea kushirikiana na jamii kwenye suala la ulinzi na usalama huku Kamanda wa Polisi mkoani Geita SACP Safia Jongo akieleza kuwa mafunzo hayo yameendelea kuwawezesha vijana kushiriki kwenye ulinzi huky yakisaidia kupunguza uhalifu katika maeneo yanayozunguka mgodi na Jamii kwa ujumla.

Mkurugenzi mtendaji wa GGML Ashraf Suryaningrat akihutubia wakati wa kuhitimisha mafunzo ya polisi jamii. Picha na Ester Mabula

Mgeni rasmi Mkuu wa wilaya ya Chato Mhe. Louis Bura kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Geita amesema ni vyema wawekezaji wengine kushirikiana na polisi pamoja na jamii kuanzisha mafunzo ya polisi jamii katika jamii zinazowazunguka huku baadhi ya wahitimu wa mafunzo hayo wakieleza faida za mafunzo waliyopata.

Mkuu wa wilaya ya Chato Mhe. Louis Bura akihutubia wakati wa kuhitimisha mafunzo ya polisi Jamii. Picha na Ester Mabula

Kwa mujibu wa kamanda wa polisi mkoa wa Geita SACP Safia Jongo ameeleza kuwa mafunzo hayo yamekuwa chachu ya kuwawezesha vijana kujipatia kipato halali, kujenga uzalendo sambamba na kujiepusha na vitendo vya uvunjifu wa amani, uhalifu, wizi pamoja na ukatili wa kijinsia.

Kamanda wa Polisi mkoaa wa Geita SACP Safia Jongo akizungumza wakati wa kuhitimisha mafunzo ya polisi Jamii. Picha na Ester Mabula
Sauti ya taarifa kwa kina kutoka kwa Ester Mabula