Storm FM
Storm FM
11 November 2025, 16:55

Mkandarasi wa mradi huo hatapewa muda wa nyongeza baada ya siku 100 kukamiliza mapema mwezi wa pili mwaka kesho.
Na Mrisho Sadick:
Wananchi wa Mtaa wa Mwatulole Manispaa ya Geita Mkoani Geita wameiomba serikali kuendelea kumsukuma mkandarasi anayetekeleza mradi wa TACTIC wa ujenzi wa barabara za lami zenye urefu wa kilometa 17 wenye thamani ya zaidi ya shilingi Bilioni 22 kwakuwa ameshindwa kukamilisha kazi hiyo kwa wakati.
Wakazi hao wakiwakilishwa na Charles William na Simon Magesa wametoa wito huo leo Novemba 11,2025 baada ya Mkuu wa Mkoa wa Geita Martine Shigela kutembelea nakukagua Utekelezaji wa mradi huo ambao hapo awali ulikumbwa na Changamoto Kutoka kwa mkandarasi hali ambayo imefanya kuchelewa kukamilisha.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo Mhandisi Mshauri Rechnold Manyanga amesema mradi huo ulianza kutekelezwa tangu mwaka 2023 lakini kutokana na changamoto kutoka kwa mkandarasi umeshindwa kukamilika kwa wakati hadi serikali ilipochukua hatua kali huku akizitaja barabara hizo na asilimia ya utekelezaji wake mbele ya mkuu wa mkoa wa Geita.

Mkuu wa Mkoa wa Geita Martine Shigela baada ya kutembelea nakukagua mradi huo amemtaka mkandarasi kuhakikisha anakamilisha kazi hiyo ndani ya siku 100 kwakuwa anatakiwa kukabidhi mradi tarehe 08-02-2026.
Katika hatua Nyingine Mkuu wa Mkoa wa Geita ametembelea ujenzi wa vyumba saba pamoja na vyoo wenye thamani ya zaidi ya milioni 100 katika shule ya msingi Nyantindili Kata ya Nyankumbu na mwalimu mkuu wa shule hiyo Helena Nemes akatoa taarifa mbele ya mkuu wa mkoa.

Mkuu wa mkoa wa Geita Martine Shigela mbali nakuridhishwa na ujenzi wa madarasa hayo ameahidi kuchangia tofali 2000 kwa ajili ya ukamilishaji wa madarasa huku akiwataka wananchi na viongozi wa serikali za mitaa kuhakikikisha wanayalinda maeneo ya shule ili yasivamiwe na shughuli za kibinadamu ikiwemo makazi.